Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amekagua vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Manispaa Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na Halmashauri ya Mji wa Bunda na kupongeza kazi inayoendelea.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali, Mheshimiwa Mzee ameeleza kazi inayoendelea ni nzuri sana na kuwapongeza mafundi na wasimamizi wa miradi hiyo katika ngazi mbalimbali katika ujenzi huo.
“Ninawapongeza kwa kuwa kazi inayofanyika ni nzuri sana, inaonekana hata kwa macho na niwaombe tu tukamilishe kazi hii kwa ubora na wakati” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewataka Wakurugenzi kujenga ofisi za walimu katikati ya vyumba vya madarasa ili kupunguza tatizo la uhaba wa ofisi za walimu katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee pia amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika ujenzi wa vyumba vya madarasa wanavyoendelea kujenga katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mara.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Shule za Sekondari kubuni na kuanzisha miradi midogo midogo katika maeneo yao ili kuweza kupata fedha za kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kutumika kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
“Miradi hiyo inaweza kuwapa fedha za kutatua changamoto ambazo bila ya fedha hizo haziwezi kutatuliwa kiurahisi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira yenu ya kazi” alisema Mheshimiwa Mzee.
Katika Manispaa ya Musoma Mheshimiwa Mzee ametembelea Shule ya Sekondari ya Baruti (madarasa 4) na Shule ya Sekondari ya Morembe (madarasa 4) na kukuta ujenzi ukiwa unaendelea katika hatua za maboma na Jeshi la Magereza likiwa limepatiwa zabuni hizo.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mheshimiwa Mzee ametembelea Shule ya Sekondari ya Mmazami ambayo awali ilipewa vyumba 13 vya madarasa lakini kutokana na uhaba wa eneo, vyumba 06 vinajengwa katika eneo hilo na vyumba 07 vinajengwa katika eneo la Sekondari mpya ya Kirumi.
Katika Halmashauri wa Mji wa Bunda, Mheshimiwa Mzee amekagua Shule ya Sekondari ya Dkt. Nchimbi ambayo imepewa vyumba 10 vya madarasa na kwa sasa ipo katika hatua ya kujenga msingi na ujenzi unatekelezwa na Jeshi la Magereza.
Katika ziara hiyo pia, Mkuu wa Mkoa amezungumza na wanafunzi wa Kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Baruti na kuwataka wanafunzi kujifunza kwa juhudi ili waweze kutumia muda huo kuboresha maisha yao ya baadaye.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambata na na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Benjamin Oganga, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Richard Moshi na watumishi wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri zilizotembelewa.
Vyumba vya madarasa vilivyokaguliwa leo ni sehemu ya vyumba vya madarasa 546 vinavyojengwa katika shule za Sekondari 144 katika Mkoa wa Mara yenye thamani ya shilingi 10,920,000 kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Mkoa wa Mara umepanga kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo mwanzoni wa Desemba, 2022 kabla kufika tarehe ya mwisho iliyowekwa na Serikali ya ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa