Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo tarehe 24 Desemba, 2022 amekabidhi zawadi za sikukuu kwa wahanga wa ukatili wanaoishi katika Kituo cha ATFGM Masanga Wilayani Tarime zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mheshimiwa Mzee amemshukuru sana Rais Samia kwa kuwakumbuka wahanga wa ukatili wanaoishi katika kituo hicho na kuwataka wahanga hao kuendelea kumuombea Rais Samia afya njema ili aendelee kuwahudumia Watanzania.
“Mheshimiwa Rais amenituma kuwaletea mkono wa kheri (zawadi) kwa ajili ya sikukuu zilizo mbele yetu za Krismasi na Mwaka Mpya” alisema Mheshimiwa Mzee na kumshukuru Rais kwa kitendo chake cha kutoa zawadi za sikukuu kwa vituo vingi hapa nchini.
Akiwa katika kituo hicho, Mheshimiwa Mzee amekemea wananchi wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto wadogo wasio na hatia kwa kisingizio cha mila zilizopitwa na wakati na kusema ukatili huo hauna tija kwa maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ametumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa kituo hicho kwa jitihada za kuwasaidia watoto wanaokimbia majumbani mwao kutokana na vitendo vya ukatili hususan ukeketaji na ndoa za utotoni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Patrick Chandi Marwa ameeleza kuwa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara kinaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kuwatunza wahanga wa ukatili katika jamii.
“Sisi kama Chama tutakemea na kuishauri vizuri Serikali kuhusu hatua za kuchukua ili kukomesha ukatili kwa mabinti unaotokana na ndoa za utotoni na ukeketaji” alisema Mheshimiwa Chandi.
Akizungumzia zawadi iliyotolewa, Mheshimiwa Chandi ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ametoa zawadi kwa watoto hao kwa kuwa yeye na chama chake kinapinga vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto wakike.
Mheshimiwa Chandi amesema Mama Samia ametoa mbuzi 7, maharage kilo 80, mafuta na viungo mbalimbali na mchele kilo 450 kwa ajili ya wahanga hao kwa kuwa yeye kama Mama anafahamu madhara wanayoyapata watoto hao.
“Mheshimiwa Rais atakapokuja tena katika Mkoa wa Mara nitamuomba aje kutembelea kituo hiki ili kujionea mwenyewe kazi kubwa inayofanyika hapa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele ameeleza kuwa Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha inakomesha suala la ukeketaji lakini wananchi wamekuwa wakibuni mbinu mpya kila wakati kuendelea kufanya ukeketaji.
Mheshimiwa Mtenjele ameeleza kuwa mwaka huu umejitokeza ukatili mwingine kwa watoto wa kiume ambao baada ya kufanyiwa tohara salama hospitali watoto hao wanalazimishwa kupelekwa tena kwa ngariba na kufanyiwa tohara tena ya kimila.
“Jambo hili kimsingi ni ukatili wa aina yake, tumelikemea kwa nguvu zetu zote na polisi wamekuwa wakichukua hatua wanapopata taarifa za tohara hizo za kurudia na wananchi wameanza kuelewa hiyo changamoto haipo tena” alisema Kanali Mtenjele.
Aidha, Mheshimiwa Mtenjele amekishukuru sana Kituo cha AFTGM Masanga kwa msaada wanaoutoa kwa wahanga hao na hasa kwa watoto waliopo katika hatari ya kuingia kwenye ukeketaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo hicho Sista Jacqueline Gbanga Ya Bongo ameeleza kuwa kituo hicho kilianza mwaka 2008 baada ya watoto na wazazi ambao hawakupenda watoto wao kukeketwa kukimbilia katika nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki katika eneo hilo kwa ajili ya kuomba hifadhi.
Baadaye wazazi na mabinti waliendelea kuongezeka na hivyo wakaamua kuanzisha kambi kwa ajili yao na Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma likaanzisha Kituo hiki kwa ajili ya kuwahifadhi watoto na wazazi wanaokimbia.
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho kimefanikia kuwaokoa watoto 4,392 waliopita katika kituo hicho kwa nyakati tofauti tofauti.
“Kwa mwaka 2022, kituo hiki kimepokea watoto 486 na baadhi ya watoto hao tayari wameanza kuwarudisha nyumbani kwao baada ya kuzungumza na wazazi na viongozi wa vijiji na kuhakikishiwa usalama wa watoto hao baada ya kurejea majumbani kwao” alisema Sista Jacqueline.
Mkuu huyo wa Kituo ameishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa sana wanaoutoa katika Kituo cha Masanga na amemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa zawadi hizo ambazo ameeleza zitawasaidia watoto hao kupata chakula wakati huu wa sikukuu.
Katika ziara hiyo, RC aliongozana pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa na watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa