Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo ameongoza kikao cha kuwajengea uelewa wa pamoja baina ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara na kuitaka Wakala hiyo kuwasilisha taarifa ya vyanzo vya maji na mkakati wa kivilinda vyanzo vilivyopo ofisini kwake kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja wa viongozi ndani ya Mkoa.
“Ninataka nipewe taarifa ya vyanzo vya maji vilivyopo na mkakati wa kivilinda vyanzo hivi ili viongozi wote tuuelewe na tushiriki kulinda kwa ajili ya kuleta uhakika wa maji kwa maendeleo ya wananchi katika Mkoa wa Mara” amesema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ametoa agizo hilo baada ya baadhi ya wajumbe wa kikao hicho kulalamika kuwa kuna baadhi ya vyanzo vya maji havijatunzwa vizuri na kusababisha uharibifu wa vyanzo hivyo kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Mkuu wa Mkoa ameitaka RUWASA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira na. 5 ya mwaka 2019 ili wananchi waepuke kuharibu mazingira na vyanzo vya maji bila kujua kuwa ni kosa kisheria.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameitaka RUWASA kufuatilia miradi ya maji inayotekelezwa katika Mkoa wa Mara ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi waliohudhuria kikao hicho kuwaelimisha wananchi wanaowawakilisha ili kulinda vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake, Mhandisi wa RUWASA Mkoa wa Mara, Nuni Munjobelege ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja baina ya RUWASA, Sekretarieti ya Mkoa na viongozi mbalimbali kuhusu mwelekeo mpya wa utoaji wa huduma yam aji vijijini chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019.
Akizungumza wakati wa kutoa mada kuhusu hali ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji katika Mkoa wa Mara, Mhandisi Nuni ameeleza kuwa kwa sasa miradi yote ya maji inayotelekezwa katika Mkoa wa Mara inaendelea vizuri.
Mhandisi Nuni ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa una miradi ya maji 115 inayotekelezwa na vikundi vya watumia maji 91 vinavyoendesha miradi hiyo baada ya baadhi ya vikundi kuanza kuunganishwa ili kuendana na mwongozo mpya wa vikundi vya watumiaji maji katika ngazi ya jamii.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Siasa ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa baadhi ya taasisi za serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa