Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenarali Suleiman Mungiya Mzee leo ameipongeza Idara ya Afya ya Mkoa wa Mara kwa kufanikisha awamu ya pili ya chanjo ya polio kwa Watoto chini ya miaka mitano iliyofanyika hapa nchini kuanzia Mei 18-22, 2022.
Mheshimiwa Mzee ametoa pongezi hizo leo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Mara mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya polio yam atone kwa awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza tarehe 1-4 Septemba, 2022.
“Katika awamu ya pili Mkoa ulichanja Watoto 630,897 ambao ni sawa na asilimia 119 ya Watoto 529,725 ya Watoto waliotarajiwa kuchanjwa katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Amewataka viongozi na watendaji wote kuongeza juhudi katika kampeni na utekelezaji wa zoezi la chanjo kwa awamu ya tatu ili Mkoa uweze kufanya vizuri zaidi katika zoezi hilo kwa kutumia fedha zilizopokelewa.
Mheshimiwa Mzee amewaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia awamu ya tatu ya chanjo katika Wilaya zao ili zoezi hili liweze kufanikiwa katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu y Afya Dkt. Juma Mfanga ameeleza kuwa hii ni awamu ya tatu kwa Tanzania kufanya zoezi la chanjo ya polio kwa Watoto wa chini ya miaka mitano baada ya ugonjwa huo kugundulika katika nchi ya Malawi Februari, 2022.
“Kwa awamu ya kwanza ilihusika mikoa michache iliyopo jirani na nchi ya Malawi na awamu ya pili ilikuwa nchi nzima na sasa inafanyika tena nchi nzima kwa watoto wote chini ya miaka mitano” alisema Dkt. Mfanga.
Dkt. Mfanga amewataka wajumbe wa kikao hicho kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi waweze kulipokea zoezi hilo vizuri na kutoa ushirikiano kwa maafisa wa chanjo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mara Bibi Flowina Muuzaje ameeleza kuwa Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) watafanya kampeni ya siku nne.
Bibi Muuzaje ameeleza kuwa katika kipindi hicho kampeni itafanyika nyumba kwa nyumba na katika maeneo yote yenye watoto wa chini ya miaka mitano ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya kama ilivyofanyika wakati wa awamu ya pili.
Aidha Bibi Muuzaje ameeleza kuwa Mkoa bado unaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wananchi, matangazo, vipeperushi na mitandao ya kijamii.
Kikao cha Afya ya Msingi Mkoa wa Mara kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Halmashauri pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa