Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amehudhuria kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2022/2023 na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kwa kupata hati safi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mhe. Mtambi ametoa pongezi hiyo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kuipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa muda wa miaka minne mfululizo.
“Hii inaonyesha kuwa mifumo ya usimamizi ye Menejimenti ya Halmashauri hiyo na Baraza la Madiwani lipo imara katika kuisimamia Halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kuongeza juhudi na weredi ili Halmashauri iendelee kupata hati safi kwa miaka inayofuata na kuendelea kupunguza hoja za ukaguzi na hususan zinazoweza kupata majibu.
Aidha, Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kukusanya shilingi 1,743,111,105 hadi kufikia tarehe 30 Mei, 2024 ambayo ni sawa na asilimia 87.48 ya lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Ni imani yangu kuwa kwa kipindi hiki kilichosalia mtafika na kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani ili kuwawezesha kutekeleza mipango ya maendeleo iliyokasimiwa katika kipindi hicho” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kukamilisha utekelezaji wa maagizo sita ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) ya tarehe 21 Juni, 2022 ambayo Halmashauri haijafanikiwa kukamilisha utekelezaji wake na kulitaka Baraza la Madiwani kusimamia uandaaji wa mpango kazi wa kuhakikisha maagizo na hoja zote zinafanyiwa kazi kikamilifu.
Kanali Mtambi amelitaka Baraza la Madiwani kuwawajibisha watumishi wote waliosababisha hoja za ukaguzi na kusimamia ukamilishaji wa miradi viporo iliyopo katika Halmashauri hiyo ili wananchi wapate huduma.
Mhe. Mtambi ameagiza manunuzi yote yafanyike kupitia mfumo wa Manunuzi ya Umma (NEST) na madiwani na watumishi wote wapewe mafunzo kuhusu mfumo wa NEST, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kanuni zake.
Aidha, amelitaka Baraza la Madiwani kusimamia mgawanyo wa mali na madeni kati ya HAlmashauri ya Wilaya ya Butiama na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mheshimiwa Moses Kaegele amepongeza ushirikiano uliopo katika ya Baraza la Madiwani, Menejimenti ya Halmashauri na watumishi wote wa Halmashauri unaosaidia katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Mhe. Kaegele amesema Halmashauri hiyo kwa sasa imepiga hatua kubwa katika kujibu hoja za CAG na kuwataka wataalamu waendelee kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuongeza bidii na ubunifu katika shughuli zao.
Taarifa ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri hiyo ilipata hati safi na ilikuwa na hoja 42 kati ya hizo hoja 16 zilikuwa za miaka ya nyuma na hoja za mwaka wa fedha 2022/2023 ilikuwa na hoja 26 huku maagizo sita ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC).
Aidha, taarifa hiyo imeonyesha kuwa Halmashauri hiyo ilikuwa pia na hoja za mfuko wa wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu na hoja za Mfuko wa Afya wa Pamoja (HSBF) ambazo utekelezaji wake bado unaendelea.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya hoja zote zilizokuwepo, hoja 16 zimehakikiwa na kufungwa na CAG na kati ya zilizofungwa na hoja 12 ni za mwaka 2022/2023 na hoja nne ni za miaka ya nyuma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa