Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameipokea na kuzungumza na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyopo katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Mtanda ameleza kuwa Mkoa wa Mara unazalisha madini mengi na ni Mkoa wa Pili Tanzania katika uzalishaji wa dhahabu.
“Tuna migodi kila wilaya ya wachimbaji wa kati na wachimbaji wadogo na uchumi wa Mkoa unategemea kwa kiwango kikubwa shughuli za uchimbaji wa madini na utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameiomba Wizara kuangalia uwezekano wa kuileta Kamati hiyo wakati mwingine kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo ili kuweza kupata picha halisi za uchimbaji wa madini na changamoto za wachimbaji wadogo wa madini katika Mkoa wa Mara.
Aidha, Mhe. Mtanda ameipongeza ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano anaoutoa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na viongozi wengine katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. David Mathayo David, ambaye pia ni mbunge wa Same Magharibi, ameshukuru kwa mapokezi mazuri ya kamati na kuahidi kuutembelea tena Mkoa wa Mara wakati mwingine.
Mhe. Mathayo ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
Kamati hiyo imeambatana na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, Maafisa wa Wizara ya Madini na maafisa kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi wengine waliokuwepo katika mapokezi hayo ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa