Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo tarehe 10 Oktoba, 2022 ametembelea Mgodi wa Dhahabu wa Kunanga uliopo katika eneo la Kinyambwiga, Wilaya Bunda na kuruhusu uchimbaji wa madini katika mgodi huo uendelee.
Mheshimiwa Mzee ametoa kibali hicho kufuatia baadhi ya wamiliki wa ardhi wa eneo hilo kuingia makubaliano na mikataba na mmiliki wa lesseni za uchimbaji katika eneo hilo na kuruhusu uchimbaji kuendelea bila migogoro iliyokuwepo hapo awali.
“Nimetoa kibali muendelee na shughuli za uchimbaji hapa kwa kufuata sheria na taratibu za uchimbaji wa madini zilizowekwa na Serikali” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, amemtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu kutoa elimu kwa wachimbaji hao kuhusu sheria na taratibu mbalimbali za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wote wa eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa pia amewataka wananchi ambao hawajakubaliana na mwenye lesseni ya uchimbaji katika eneo hilo, kuendelea na shughuli zao za kawaida bila kubughudhiwa na mwenye lesseni.
Mheshimiwa Mzee pia ametoa siku saba kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2022 kwa wachimbaji wadogo kusajiri mashimo, klasha na maduala kwa mujibu wa sheria na taratibu za madini.
Mheshimiwa Mzee ameiagiza Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda pamoja na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kusimamia usajiri huo kabla ya kuendelea kuchimba madini katika eneo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Guta Mheshimiwa Kigno Nyakimori ameeleza kuwa kwa sasa wachimbaji wa eneo hilo wanaishi maisha magumu kufuatia kufungwa kwa mgodi huo na kumuomba Mkuu wa Mkoa kuruhusu uchimbaji uendelee.
Mheshimiwa Nyakimori ameeleza kuwa wananchi waliokataa kuingia makubaliano na mwenye lesseni ya uchimbaji wamefanya hivyo kwa kuwa wanataka haki itendeke maeneo yao yakitumika na mwenye lesseni ya uchimbaji.
Ameeleza kuwa wananchi hao walianzisa vurugu baada ya kuona hamna muafaka na mwenye lesseni lakini kutokana na makubaliano yaliyofikiwa hategemei kuwa na vurugu tena katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mzee amewataka wachimbaji hao kutodanganyika na watu wanaopita na kuwapotosha kuhusiana na mmiliki wa lesseni za madini na uhalali wake wa kuchimba madini katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa, Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Bunda, maafisa kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Serikali ya Mkoa wa Mara iliufunga mgodi huo tarehe 13 Aprili, 2022 kufuatia vurugu iliyokuwa imejitokeza na wananchi kumjeruhi askari polisi baada ya polisi kufika eneo hilo kutuliza vurugu zilizokuwepo na baadhi ya wananchi kuwashambulia.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa