Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo amefungua rasmi kikao cha Kitaifa cha maafisa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu maandalizi ya Siku ya Mara (Mara Day) ambayo yanatarajia kufanyika tarehe 12-15 Nakuru, nchini Kenya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mheshimiwa Mzee amewataka maafisa kutoka taasisi mbalimbali zilizohudhuria kikao hicho kutekeleza kwa vitendo maamuzi ya kutunza mazingira katika maeneo yote kuzunguka Mto Mara.
“Mimi ninataka maadhimisho haya yawe yanaacha alama kwa kupanda miti ya kutosha na kulinda miti iliyopandwa ili kuacha alama ya kudumu kwa wananchi wa Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee pia amewataka maafisa hao kufanya maandalizi mapema ya Siku ya Mara na kutoa hamasa zaidi kwa wananchi kushiriki hususan katika kupanda miti na kutunza miti yote itakayopandwa katika maadhimisho hayo.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na historia ya maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Bwana Eliabi Khalid Chodota ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa kisekta la Bonde la Ziwa Victoria uliofanyika tarehe 4 Mei, 2012 Kigali, Rwanda.
“Maadhimisho haya hufanyika kwa lengo la kutoa msukumo kwa hifadhi ya bonde la Mto Mara unaoanzia milima ya Mau nchini Kenya na kuishia Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania” alisema Bwana Chodata.
Bwana Chodota ameeleza kuwa maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kuanzia mwaka 2012 kila mwaka na kilele cha maadhimisho hay ani tarehe 15 Septemba ya kila mwaka hii ikihusiana na uhamaji wa Wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania Kwenda Maasai Mara nchini kenya kwa ajili ya malisho na baadaye kurudi kuzaliana katika Hifadhi ya Serengeti.
Kikao cha Kitaifa cha maandalizi ya Siku ya Mara kilihucdhuriwa pia na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Ofisi za Bonde la Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, baadhi ya maafisa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Maafisa Mazingira na maafisa Maendeleo ya Jamiiwa Halmashauri za Mkoa wa Mara.
Baada ya kikao hicho, kikao cha kimataifa cha maandalizi ya Siku ya Mara kilifanyika kwa njia ya mtandao na kuwahusisha maafisa kutoka nchi za Kenya, Tanzania na Mashirika ya Kimataifa yanayohusiana na mazingira, maji na uhifadhi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa