Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Sulaiman Mzee leo tarehe 16 Agosti, 2022 amefanya ziara ya kujitambulisha katika Wilaya ya Musoma na kuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuwasilisha maelezo ofisini kwake kwa nini miradi ya ujenzi imesimama.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri na Hospitali ya Hamashauri ya Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Mzee ameutaka uongozi ya Halmashauri hiyo kuwa kutoa maelezo ya kina kwa nini miradi hiyo.
“Ninataka maelezo ya kina kwa nini miradi hii imesimama na fedha za ujenzi wa miradi hii zipo kwa muda mrefu lakini ujenzi hauendelei na wala haujakamilika” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee aliagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika wote wa ujenzi wa jengo la Halmashauri baada ya kupewa taarifa kuwa kutokana na upotevu wa nondo 1,026 katika mradi huo, maafisa wote waliowekwa ndani wamepewa dhamana na Mtunza Stoo tu ndiye anashikiliwa na polisi.
Mkuu wa Mkoa aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuendelea kukamilisha miradi hiyo kwa haraka ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Msongela Nitu Palela ameeleza kuwa miradi hiyo imesimama kutokana na uchunguzi unaofanyika kufuatia wizi wa nondo kubainika katika mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo.
“Tumeunda tume ambayo inafanyakazi kwa siku tatu kukagua vifaa vyote vilivyoko kwenye stoo ili kujiridhisha baada ya kubaini wizi huo wa nondo katika mradi wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri” amesema Palela.
Bwana Palela ameeleza kuwa kwa sasa miradi yote imesimama kufuatia uchunguzi unaoendelea na kukosekana kwa mtaalamu wa stoo ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi kufuatia wizi huo.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mzee ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma na baadaye miradi ya ujenzi ya ofisi za Halmashauri na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya, ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Musoma vijijini na jengo jipya la CCM linalojengwa Musoma vijijini.
Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma na viongozi wengine wa CCM wa Wilaya ya Musoma.
Huu ni mwendelezo wa ziara za Mkuu wa Mkoa tangu alipoteuliwa kuja Mara na kuanza kazi tarehe 6 Agosti, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa