RC AAGIZA UCHUNGUZI WA MIRADI RORYA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuunda kamati ya kuchunguza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea baadhi ya miradi na kushiriki katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujibu Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) leo tarehe 15, 2022.
“Nitataka Katibu Tawala uunde timu ya uchunguzi itusaidie kuchunguza miradi yote ambayo haijatekelezwa vizuri na inayolalamikiwa na wananchi wa Wilaya ya Rorya ili kujiridhisha” alisema Mheshimiwa Hapi.
Miradi itakayochunguzwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya, jengo la ofisi za Halmashauri, ukumbi wa Halmashauri pamoja na ujenzi wa kivuko cha watembea kwa mguu katika daraja la Mto Mori kilichotekelezwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya, ililetewa fedha za kujenga majengo saba ya awali bilioni 1.5 ambazo ziliisha bila majengo kukamilika na serikali iliongeza tena milioni 300 lakini majengo hayo mpaka leo hayajakamilika.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Hospitali hiyo pia ililetewa shilingi milioni 500 za kujenga wodi tatu lakini fedha zimeisha lakini majengo hayo hayajakamilika.
Mheshimiwa Hapi pia amebaini gharama za mafundi wa kujenga wodi hizo ni asilimia 20 ya vifaa vyote jambo ambalo ni kinyume na mwongozo wa serikali wa asilimia 15 ya gharama za vifaa.
Akiwa katika Hospitali hiyo, pia Mheshimiwa Hapi amekagua mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa hospitali hiyo three in one ambao upo katika hatua za ukamilishaji na mradi wa ujenzi wa mochwari, wodi nyingine ambao upo katika hatua za utekelezaji.
Mheshimiwa Hapi ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kufanya mapitio ya mpango wa matumizi ya ardhi katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya na kuomba idhini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili hospitali hiyo isiendelee kujenga miundombinu mingine kwenye eneo lenye maji maji wakati eneo zuri lipo.
Mkuu wa Mkoa pia ametembelea jengo la ofisi za Halmashauri pamoja na ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambao ulianza kujengwa mwaka 2007 na SUMA JKT hata hivyo jengo la ofisi linatumika wakati ukumbi ulisimama kutokana na kuishiwa fedha na kuanza kujengwa tena mwaka 2022 baada ya Serikali kuleta fedha milioni 750 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Hapi ameikemea Halmashauri hiyo baada ya kutaarifiwa kuwa Halmashauri hiyo imeomba fedha za nyongeza milioni 250 kukamilisha jengo hilo; “kwa hatua hii mlipofikia na fedha mnayosema imebakia, mnahitaji shilingi milioni 250 kwa ajili ya nini?” alisema Mheshimiwa Hapi.
“Hili jengo (ofisi za Halmashauri) mpaka leo halijakamilika, kuna jenerata na strongroom kwa ajili ya kuhifadhia mitihani ilitakiwa kuwekwa havijawekwa, vigae vimebanduka na halijakabidhiwa muda wote huo” alisema Mhehsimiwa Hapi.
Kuhusu kivuko, Mheshimiwa Hapi amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wanaolalamikia kivuko hicho kutumia gharama kubwa ukilinganisha.
“Ninataka hiki kivuko nacho tukichunguze kujua uhalali wa kutumia zaidi ya milioni 70 katika kivuko hicho ambacho wananchi wanakilalamikia” alisema Mheshimiwa Hapi.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa, Mhandisi wa Halmashauri hiyo Mhandisi Erick Mwita ameeleza kuwa awali hospitali hiyo ililetewa kiasi cha bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga majengo saba ambayo hayakukamilika na baadaye ikaletewa shilingi milioni 300 kukamilisha lakini bado majengo hayo hayajakamilika.
Mhandisi Mwita ameeleza kuwa baadaye Hospitali hiyo ilipokea fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga wodi tatu ambazo pia hazijakamilika, vifaa vimenunuliwa lakini hamna fedha za kulipa mafundi ili kuendelea na kazi.
“Katika ujenzi wa wodi hizi, Halmashauri ilipata gharama kubwa ya kuleta vifaa eneo la ujenzi wakati wa masika kutokana na ubovu wa barabara na msingi kutumia fedha nyingi kutokana na eneo kuwa na maji maji” alisema Mhandisi Mwita.
Aidha, Mhandisi Mwita ameeleza kuwa serikali imeleta tena fedha nyingine kwa ajili ya kujenga majengo mengine ambapo ujenzi wake unaendelea.
Akiwa katika Kikao cha Baraza la Madiwani, Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri hiyo kukusanya madeni na kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo. Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja 68 na hoja 10 zilijibiwa na kufungwa, hoja nyingine zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa