Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuunda timu ya kuchunguza uhalisia na uhalali wa madeni katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Julai, 2022 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/2021.
“Nataka timu ije kuchunguza uhalisia na uhalali wa deni lenye thamani ya bilioni 4.1 linalosemekana lipo katika Halmashauri ili kubaini limetokana na nini, uhalali wake ili kama Mkoa tujiridhishe na deni hili” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha timu inayokagua miradi iliyokwama katika Halmashauri ipite na Kituo cha Afya Machochwe kilicholetewa fedha milioni 500 ambazo zimeisha na kituo hakijakamilika.
“Ninataka uchunguzi katika huo mradi, nchi nzima milioni 500 zinakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya, lakini Serengeti wanasema zimeisha na zinahitajika nyingine milioni 150 kukamilisha mradi huo, hii haikubaliki” alisema Mheshimiwa Hapi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa ameipongeza Shule ya Sekondari ya Natta kwa kushika nafasi ya 11 kitaifa kwenye matokeo ya Kidato cha Sita ya mwaka 2022 yaliyotangazwa hivi karibuni.
“Mimi nitatoa shilingi 500,000 kwa ajili ya kuwapongeza walimu, lakini ninataka Mkuu wa Wilaya ongea na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Natta kwa kufanya vizuri” alisema Mheshimiwa Hapi.
Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Ayoub Mwita Makuruma ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ina madeni makubwa yaliyosababisha na uzembe wa viongozi waliokuwepo katika Halmashauri hiyo.
“Cha kushangaza kuhusu haya madeni kwa sehemu kubwa yametengenezwa katika kipindi ambacho Halmashauri hiyo ikiwa katika hali nzuri kifedha, jambo ambalo linazua maswali kwa nini hayakulipwa” ameeleza Mheshimiwa Makuruma.
Ameelezea wasiwasi wa madeni hayo kuwa huenda yalitengenezwa tui li kuchukua fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mheshimiwa Makuruma amemuomba Mkuu wa Mkoa kuisaidia Halmashauri hiyo kwa kuwaondoa wakuu wa Idara na Vitengo waliokaa katika nafasi zao kwa muda mrefu.
Suala la madeni liliongelewa pia na madiwani waliopata nafasi ya kuchangia katika kikao hicho na kuonyesha kutoridhika kwao na deni hilo la Halmashauri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bwana Kivuma Msangi ameeleza kuwa Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa ina hoja 93 na hadi wakati wa kikao hicho 31 zilikuwa zimejibiwa na zimefungwa, hoja 29 zinazoendelea kujibiwa na hoja nyingine 33 hazijaanza kutekelezwa.
Bwana Msangi ameeleza kuwa Halmashauri pia ilikuwa na maagizo mawili ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) ambapo moja limejibiwa kikamilifu na moja linaendelea kujibiwa kipengele kinachohusu mwekezaji Grumeti kulipa ada ya uwindani milioni 500 badala ya milioni 200 wanazolipa sasa.
Bwana Msangi ameeleza kuwa katika ukaguzi huo Halmashauri hiyo ilipata hati safi ya ukaguzi na hiyo ni mwendelezo ambapo kwa miaka mitatu mfulilizo imekuwa ikipata hati safi za ukaguzi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Serikali za Mitaa, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa na Wilaya, wajumbe wa Baraza la Madiwani, Wakaguzi kutoka ofisi ya CAG, watumishi wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa