Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara kuanza kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wa watoto ambao wanatakiwa kwenda shule lakini hawajapelekwa.
Mheshimiwa Mzee ametoa agizo hilo leo katika eneo la Nyamswa katika Wilaya ya Bunda baada ya kupokea taarifa za usajiri wa wanafunzi usioridhisha katika Wilaya ya Bunda hadi tarehe 11 Januari, 2023.
“Ninataka kuona watoto wote wamepelekwa shule au wazazi wawe wamechukuliwa hatua za kisheria na nipate taarifa ya utekelezaji wa agizo hili” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amesema haitavumilika kuona Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na kuweka walimu huku wazazi wakikwamisha jitihada za Serikali za kuboresha elimu hapa nchini.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewaagiza wasimamizi wa elimu katika Mkoa wa Mara kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wanapoenda shule.
Awali, Mheshimiwa Mzee aliwauliza wanafunzi wa shule za msingi mbalimbali kutoka katika Tarafa ya Chamriho waliohudhuria hafla hiyo maswali ya uelewa na kutoa shilingi 10,000 kwa ambaye angeweza kujibu maswali hayo, lakini hamna aliyeweza kujibu kwa usahihi.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewataka Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuboresha mazingira ya shule na sehemu nyumba za walimu zilizopo katika mazingira ya shule ili wanafunzi waweze kujifunza sio tu masomo ya darasani lakini hata namna nzuri ya kuishi kwenye mazingira masafi.
“Mwanafunzi akija shule mbali ya masomo anajifunza kutoka kwa walimu na watu wengine wanavyovaa, wanavyoishi, wanavyoongea na wanavyofanya mambo yao, hivyo walimu wakiwa wanaishi katika mazingira ya hovyo, wanafunzi wanakuwa hawana cha kujifunza” alisema Mheshimiwa Mzee.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mheshimiwa Joshua Nassari ameeleza kuwa katika Wilaya hiyo usajiri wa wanafunzi ni mdogo katika Halmashauri zote mbili pamoja na Wilaya kuchukua hatua za kuwawezesha wazazi kuwapeleka watoto shule.
“Katika Wilaya ya Bunda tumeruhusu wazazi kuwapeleka watoto shule hata wasipokuwa na sare za shule au michango ya shule ili watoto waweze kuanza masomo yao lakini bado wanafunzi wachache wameandikishwa mpaka sasa” alisema Mheshimiwa Nassari.
Mheshimiwa Nassari ametolea mfano wa Kata ya Nyamswa ambapo kati ya wanafunzi 392 waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza, wanafunzi 90 tu walikuwa wamepokelewa shuleni mpaka tarehe 11 Januari, 2022.
Mheshimiwa Nassari ameeleza kuwa katika Wilaya ya Bunda wametoa siku saba wazazi wote wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule wame wamepelekwa shule na baada ya hapo wataanza kuchukua hatua za kisheria.
Aidha, Mheshimiwa Nassari ameeleza kuwa katika fedha zilizotolewa mwaka 2022 za ujenzi wa madarasa Wilaya ya Bunda ilipata Bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Halmashauri zake zote mbili.
“Kwa sasa Wilaya ya Bunda inamadarasa ya kutosha kwa shule za sekondari na katika baadhi ya maeneo kuna ziada ya vyumba vya madarasa” amesema Mheshimiwa Nassari.
Shule za msingi na sekondari zilifunguliwa tarehe 9 Januari, 2022 hapa nchini na hadi sasa usajiri wa wanafunzi wapya unaendelea katika shule zote hapa nchini.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, viongozi na maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa