Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amefungua mafunzo ya siku tatu kwa Walimu Wakuu 140 na Maafisa Elimu Kata 30 wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuwataka wasimamizi wa elimu katika ngazi mbalimbali kutimiza wajibu wao.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Bwana Makungu amewataka walimu kujitathmini ni vitu gani wanajivunia katika utumishi wao na kuwataka kusimamia maadili ya walimu na wanafunzi wanaowalea ili kujenga Taifa lenye maadili mazuri.
“Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata tukitimiza wajibu wetu vizuri kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule zetu, walimu watabadilika katika kufundisha wanafunzi na wanafunzi wataongeza juhudi kwa kuwa wanafuatiliwa na walimu wao” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amewataka Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata kuimarisha mawasiliano baina yao na wanaowaongoza na wasimamizi wa elimu katika ngazi za Halmashauri na Mikoa ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili walimu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti haijafanya vizuri sana kwenye matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba wa mwaka 2023 na mafunzo haya yawe chachu ya kuboresha ufaulu.
Bwana Makungu amewaacha Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata kuacha kusimamia kwa mazoea bali wasimamie kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia Sekta ya Elimu hapa nchini.
“Mkisimamia kwa mazoea ndio mwanzo wa kutengeneza msingi wa hoja ya kuondolewa kwenye madaraka mliyonayo”amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amewakumbusha umuhimu wa Walimu Wakuu kuwashirikisha wlaimu wote katika utendaji wao na kuancha kutengeneza makundi kati ya watumishi waliopo ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Bwana Samwel Mwita ameeleza kuwa awali walibaini changamoto ya uongozi katika shule za msingi na Maafisa Elimu Kata na Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM) walikubali kutoa mafunzo ya uongozi katika ngazi hizo.
“Imebainika kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuna changamoto nyingi za kiuongozi kuliko Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara na ninaamini baada ya mafunzo haya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti itabadilika kwa maana ya uongozi na usimamizi wa elimu” amesema Bwana Mwita.
Aidha, Bwana Mwita amewakaribisha wakufunzi kutoka Adem Mbeya, Bagamoyo na Mwanza na maafisa kutoka Benki ya Dunia ambao wamekuja kuangalia namna mafunzo yanavyoweza kuleta matokeo chanya kwa viongozi.
Bwana Mwita ameeleza kuwa mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti tu ndio itakayopatiwa mafunzo hayo, lakini Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara zitapatiwa mafunzo kama hayo mwakani.
Akitoa neno la shukrani Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage B, Mwal. Maswi Chacha ameishukuru Serikali na Mradi wa Shule Bora kwa kuandaa mafunzo hayo kwa Walimu na Maafisa Elimu Kata na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.
“Kwa niaba ya walimu wenzangu, ninaahidi tutashiriki kikamilifu katika mafunzo haya na kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi na wakufunzi” amesema Bwana Chacha.
Bwana Chacha ameahidi watajitahidi kusimamia ufundishaji na ujifunzaji ili matokeo ya mitihani inayokuja iwe na mabadiliko chanya.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa pia na baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa