Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo tarehe 9 Desemba, 2023 ametoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utafiti unaoendelea katika Mkoa wa Mara wa kukusanya taarifa za shughuli za Kijamii na Kiuchumi wa mwaka 2023/24 unaofanywa na Serikali katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
“Niwaombe wananchi wote wa Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano kwa utafiti unaoendelea ili Serikali iweze kupata taarifa sahihi zitakazoiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi na kutunga sera sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa utafiti huo unafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na unafanyika katika mikoa yote kwa siku 90 kuanzia tarehe 6 Desemba, 2023.
“Taarifa za takwimu zinazokusanywa ni siri kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura ya 351 na zinatumika kwa malengo mahususi ikiwa ni pamoja na maandalizi ya sera na kufanya maamuzi kwa maendeleo ya Taifa” amesema Bwana Makungu.
Kwa mujibu wa Bwana Makungu, matokeo ya utafiti huu yatawezesha kufanyika kwa uchambuzi wa kina wa hali ya kiuchumi, kupima tija katika uzalishaji na kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Baadhi ya maswali yatakayoulizwa na wadadisi wa utafiti huo ni pamoja na jina la shughuli, mahali ilipo, anuani ya posta, namna za simu, uhalali wa umiliki, mwaka shughuli ilipoanza kufanya kazi, usajiri wa shughuli husika, idadi ya watumishi, jumla ya mapato kwa mwaka.
Bwana Makungu ameeleza kuwa utafiti huu utafanyika kwa kuwatumia wadadisi kwenye maeneo ya vijijini na mijini ambao watakuwa na vitambulisho vya Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa