Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amefanya ziara Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa katika eneo la Bulamba, Wilaya ya Bunda.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Bwana Kusaya amemtaka Mkuu wa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi (MMI) kuanzisha uchunguzi wa matumizi ya fedha shilingi bilioni tatu zilizotolewa na Serikali kutekeleza mradi huo.
Bwana Kusaya amehoji sababu ya Halmashauri kununua baadhi ya vifaa kwa wingi zaidi ya mahitaji ya mradi kwa awamu hii kama vile mbao, nondo na matofali na kusababisha Halmashauri kukosa fedha za kukamilisha majengo yaliyopangwa kutekeleza katika awamu ya kwanza ya mradi huo.
Bwana Kusaya ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kukamilisha vitu muhimu vya mradi huo ili kuweza kuchukua wanafunzi 200 waliopangiwa kusoma katika shule hiyo kidato cha tano kuanzia Julai, 2024.
Aidha, Bwana Kusaya ameeleza kuwa kutokana na Halmashauri kuamua kujenga mashimo machache ya maji taka alitegemea fedha nyingi zingeokolewa katika mradi huo, hata hivyo fedha zimetumika kiasi kikubwa na mradi upo asilimia 70 huku madawati na vitanda vikiwa katika matengenezo.
Bwana Kusaya amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana George Mbilinyi kuanza mazungumzo na wananchi wanaoizunguka shule hiyo ili waweze kuhamishwa kupisha ukamilishaji wa mradi huo.
“Shule hii inategemewa kuwa ina majengo mengi sana na kwa bahati mbaya majengo yaliyopo yamejengwa ya chini na sio ghorofa, hapa lazima kupata eneo la ziada sasa wakati bado kuna nyumba chache katika eneo hili” amesema Bwana Kusaya.
Kwa upande wake, Mhandisi Thimoth Mwanjala Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ameeleza kuwa kwa sasa mradi katika awamu ya kwanza umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake huku Halmashauri ikitegemea kupata mgao wa fedha za nyongeza bilioni moja kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya shule hiyo.
Mhandisi Mwanjala ameeleza kuwa utengenezaji wa vitanda na viti utafanyika katika eneo la mradi kwa kutumia mafundi walioingia nao mkataba baada ya mzabuni kukamilisha uwasilishaji wa vifaa alivyoagizwa kwa ajili ya kutengeneza vitanda 120 na viti na madawati 200.
Bwana Mwanjala ameeleza kuwa kwa sasa Halmashauri imebakia na fedha taslimu shilingi milioni 69 na vifaa vyenye thamani ya shilingi zaidi ya shilingi milioni 180.
Mhandisi Mwanjala ameeleza kuwa Halmashauri imeshanunua senyenge kutoka Grumeti kwa ajili ya kujengea uzio wa shule hiyo na unategemewa kufungwa ndani ya wiki mbili.
Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkoa wa Mara inajengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 6, kwa awamu ya kwanza Serikali imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa, jengo la utawala, nyumba mbili za walimu, mabweni manne, maabara za sayansi na Jiografia, Bwalo la chakula, sehemu ya mapumziko kwa wagonjwa.
Shule ya Wasichana Mkoa wa Mara itakapokamilika inatarajia kuchukua wanafunzi wasichana 1,200 kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala aliambatana na Wakuu wa Sehemu, Vitengo na Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Mkurugenzi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bwana Kusaya kufanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi katika Shule ya Wasichana Mkoa wa Mara baada ya kuhamishiwa Mkoa wa Mara hivi karibuni na kuahidi kurudi tena tarehe 10 Mei, 2024 kuangalia utekelezaji wa maelekezo aliyotoa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa