Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo ameingia Mkoani Mara na kuelezea kuridhishwa kwake na mapokezi makubwa aliyoyapata ambapo kimkoa amepokelewa katika Mji wa Bunda.
“Ingekuwa hamkuja kwa wingi hivi, ningesema sijakaribishwa Mkoa wa Mara, lakini kwa kuja kwenu kwa wingi hivi mmenikaribisha katika Mkoa wa Mara, Asanteni sana” alisema Mheshimiwa Rais.
Mara baada ya kupokelewa katika Mji wa Bunda, Mheshimiwa Rais amesalimiana na wananchi wa Mji wa Bunda na baadaye kusalimiana na wananchi wa eneo la Kiabakari katika Wilaya ya Butiama.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa katika Mji wa Bunda, Mheshimiwa Rais ameshukuru kwa mapokezi makubwa aliyoyapata katika Mkoa wa Mara.
“Kwa umati huu wa watu nimefurahi tumepokelewa vizuri katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Mhehsimiwa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemkaribisha Rais katika Mkoa wa Mara.
“Wananchi wa Mkoa wa Mara wanakupenda sana na wanaridhika na kazi kubwa inayofanywa na serikali yako ya awamu ya sita” ameeleza Mheshimiwa Hapi.
“Kwa niaba ya viongozi wenzangu ndani ya Mkoa, sisi tunakupenda, tunakuamini, tunakuombea na tutakusaidia kutimiza maono yako kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Mara wanafahamu kazi kubwa anayoifanya katika Mkoa wa Mara na umati wa wananchi uliojitokeza unadhihirisha mapenzi makubwa walionayo wananchi kwa Mheshimiwa Rais na serikali yake.
Kesho tarehe 5 Februari, 2022, Mheshimiwa Rais anatarajiwa kushiriki katika Matembezi ya Mshikamano ambayo yataanzia Ikulu Ndogo ya Mkoa wa Mara hadi katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mara na baadaye Mheshimiwa Rais atakuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo kitaifa yatafanyika katika Uwanja wa Karume, Manispaa ya Musoma.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, tarehe 6 Februari, 2022 Mheshimiwa Rais anataweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mgango- Kiabakari pamoja na kuwasalimia wananchi wa eneo la Mgango lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Aidha siku hiyo Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) iliyopo katika Manispaa ya Musoma na kuzungumza na wananchi wa eneo la Kwangwa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa tarehe 7 Februari, 2022 Mheshimiwa Rais anatarajiwa kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa katika eneo la Mwitongo, Wilayani Butiama na baadaye kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa chujio la maji, katika Mradi wa Maji wa Bunda, liliopo katika eneo la Nyabehu, Wilaya ya Bunda.
Imeeleza pia kuwa Mheshimiwa Rais atahitimisha ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Mji wa Bunda katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya sabasaba.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewaalika Watanzania wote kujitokeza kwa wingi katika Maadhimisho ya Miaka 45 ya CCM ambapo Mkoa wa Mara umepewa heshima wa kuwa mwenyeji wa tukio hilo la kihistoria kwa Chama cha Mapinduzi.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tangu alivyoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 19 Machi 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa