Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 5 Mei 2020 amemaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi kati ya wakazi wa eneo la Nyamongo Wilayani Tarime na Mgodi wa Barrick North Mara.
Akitoa salamu za Rais kwa wananchi wa Nyamongo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima, amesema Mheshimiwa Rais ameridhia wananchi walipwe fidia yenye thamani ya shilingi 6,000,000 kwa ekari jambo ambalo lilipokelewa kwa furaha na wananchi wa Nyamongo.
“Mheshimiwa Rais Magufuli ameridhia mlipwe shilingi 6,000,000 kwa ekari moja baada ya kusikiliza kilio chenu cha muda mrefu sana kuhusiana na suala hili” alisema Mheshimiwa Malima.
Awali wananchi hao walitaarifiwa kuwa watalipwa fidia ya shilingi 4,200,000 kwa ekari na wakaomba serikali iongeze kiasi hicho ifike angalau milioni 6,000,000. Baada ya majadiliano kati ya wananchi na viongozi wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya alipeleka taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu maombi hayo na Mkuu wa Mkoa akawasiliana na viongozi wa serikali na Rais akaridhia ombi la wananchi.
Kufuatia makubaliano hayo Mkuu wa Mkoa wa Mara aliuagiza Mgodi wa North Mara kuandaa malipo ya fidia na kuhakikisha wananchi wa Nyamongo wanalipwa fidia zao baada ya siku 14 kuanzia tarehe 5 Mei 2020.
“Nitawaleta hapa viongozi wa serikali na Waziri wa Madini tarehe 20 Mei 2020 ili waje kusherekea na wananchi wa Nyamongo wakiwa wameshapata fedha zao” alisema Malima.
Aidha amewaagiza wananchi watakaolipwa fidia hiyo kufungua akaunti za benki ili kuwawezesha mgodi kulipa malipo hayo kwenye akaunti zao ili kupata sehemu salama ya kuhifadhi zao na kuzuia uwezekano wa wizi wa fedha hizo.
Ameeleza kuwa mgogoro huo ni tatizo la watanzania wote, kwa sasa sasa Mgodi wa Barrick umeungana na serikali na kuunda Kampuni ya Twiga ambayo serikali ya Tanzania inahisa zake na kwa maana hiyo sehemu ya mgodi huo kwa sasa ni mali ya watanzania.
“Kilichofanyika leo ni kwa maslahi mapana ya serikali, mgodi na Taifa zima” alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa Nyamongo ni eneo ambalo linautajiri mkubwa na hivyo kwa mgogoro uliokuwepo kuna watu waliokuwa wananufaika na mgogoro huo wakati wananchi walio wengi wakiwa wanaumia.
“Hapo awali uthamini wa eneo hili ulikuwa unapotoshwa na watumishi na viongozi wasio waaminifu wa serikali na mgodi kwa maslahi yao, lakini sasa hii ndio stahiki halali ya wananchi na italipwa moja kwa moja wananchi kupitia akaunti zao za benki”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri ameshukuru kwa amani na utulivu ulioonyeshwa na wananchi wa Nyamongo wakati wote wa majadiliano ya fidia hiyo.
“Tukiendelea kudai haki zetu kwa amani, utulivu na kwa kufuata utaratibu, tutapata manufaa mengi sana kutoka sehemu mbalimbali” Alisema Eng. Msafiri.
Wananchi wengi waliokuwepo katika mkutano huo walielezea kuridhishwa kwao na maamuzi ya Rais, huku diwani wa eneo hilo akiahidi kumkabidhi ng’ombe siku Rais atakapotembelea Nyamongo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Viongozi wa Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Tarime Vijijini.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kamishna wa Madini na Mthamini Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu wa Mgodi wa Barick North Mara na wajumbe wa bodi ya Kampuni ya Twiga wanaoiwakilisha Serikali ya Tanzania katika bodi hiyo.
Jumla ya wananchi 1,639 wa vijiji vya Matongo na Myabichune katika eneo la Nyamongo wanalipwa fidia na mgodi wa North Mara kwa ajili ya maeneo yao yatakayochukuliwa na Mgodi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa