Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo amechangia shilingi milioni 30 kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Jimbo Katoliki Musoma na kulihakikishia kanisa ushirikiano wa Serikali katika shughuli zake hapa nchini.
Ahadi hiyo ya Mhe. Rais imetolewa leo tarehe 29 Agosti, 2024 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius John Ndejembi (Mb), alipomwakilisha Mhe. Rais katika jubilee ya miaka 40 ya upadre na miaka 17 ya Uaskofu ya Askofu Michael Msoganzila, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma iliyofanyika Katika Uwanja wa Karume, Musoma.
“Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini bega kwa bega kuhakikisha tunatimiza adhma na malengo ya watanzania ya kuwa na maendeleo endelevu” amesema Mhe. Ndejembi.
Mhe. Ndejembi amesema Mhe. Rais ametoa fedha hizo kwa kutambua utumishi wa Askofu Msoganzila kama kiongozi wa Jimbo Katoliki la Musoma na fedha hizo zitasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kanisa katika jimbo hilo.
Akizungumza katika jubilee hiyo, Mhe. Ndenjembi amesema yeye kama Waziri pia anachangia shilingi milioni tano kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Musoma na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb.) naye akaahidi kuchangia shilingi milioni tatu na kuwataka viongozi wengine wa Serikali alioambatana nao kuchangia.
Mhe. Ndejembi amempongeza Askofu Msoganzila kwa kutimiza miaka 40 ya upadre na kumshukuru kwa kuitumia vizuri miaka hiyo kuwahudumia watu jambo ambalo amelifanya vizuri kwa miaka hiyo yote kwa kuwa tangu zamani alimweka Mungu mbele katika maisha yake kuliko matamanio ya kawaida ya kibinadamu na Mungu amemfanikisha katika maisha yake.
Akitoa mahubili katika Misa Takatifu ya kuadhimisha jubilee hiyo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo amesema maadhimisho ya miaka 40 ya upadre na miaka 17 ya uaskafu wa Askofu Msoganzila yanatukumbusha watu wote kutoa shukrani kwa Mungu kwa mema aliyotutendea katika maisha yetu.
“Katika injili tunaona watu 10 waliponywa na Yesu lakini ni mmoja tu ndiye aliyerudi kwa Bwana kumshukuru lakini wengine tisa hawakurudi tena kutoa shukrani zao” amesema Mwadhama Kadinali Pengo.
Kadinali Pengo amesema kuwa kwa shukrani ya miaka 40, Askofu Msoganzila amewakumbusha watu wote kuiga mfano wa yule mmoja aliyerudi kumshukuru Yesu baada ya kumponya na wasiwe kama wale wengine tisa ambao hawakurudi kutoa shukrani zao ingawa nao waliponywa pamoja naye.
Kadinali Pengo amewaalika watu wote kumshukuru Mungu kwa mema mbalimbali anazowajalia katika maisha yao na kuwakumbusha kuwa Mungu anapatikana popote walipo na sio lazima kufunga safari ya kumshukuru kwani anapatikana popote pale.
Ameifananisha miaka 40 na safari ya wana wa Israeli jangwani na baada ya muda huo waliweza kuingia katika nchi ya ahadi na kumuombea Mungu ampe miaka mingine zaidi ya kuishi ili aweze kuyatimiza mapenzi ya Mungu hapa duniani.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya amempongeza Askofu Msoganzila kwa kutimiza miaka 40 ya upadre.
Bwana Kusaya amesema Mkoa wa Mara unatambua na kuheshimu kazi nzuri inayofanywa na Kanisa Katoliki hapa nchini na kuahidi kuwa viongozi wa Serikali Mkoa wa Mara wataendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa hilo na viongozi wake wakati wote.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Methew amelitaka Kanisa kuendelea kuwaombea viongozi wa Serikali na taasisi nyingine hapa nchini ili waweze kutenda kazi zao kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania bila ubaguzi.
Aidha, amewataka viongozi wa Dini kuiombea nchi yetu Amani na utulivu na hususan katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Jubilei hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Metthew.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa