Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo amemuapisha Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi, Mhe. Samia amemtaka Kanali Mtambi kusimamia mpango wa Serikali kuwalipa fidia wananchi wa Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda wanaoondoka katika maeneo yao ili kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
“Tunakwenda kulipa fidia kwenye eneo moja pale Serengeti (Nyatwali) ili tukuze utali, hilo nalo nenda kalisimamie ni la muda mrefu na wananchi wamevunjika moyo, ukalisimamie liende vizuri” amesema Mhe. Samia.
Aidha, Mhe. Samia amemtaka Mhe. Mtambi kudhibiti kilimo cha bangi na usafirisha haramu wa bangi katika Mkoa wa Mara kwa kufuata Sheria za nchi.
“Kuna watu (watumishi wa Serikali) wanasindikiza magari yenye mazao (bangi) baada ya kuvuna basi watu wako Serikalini wanasindikiza magari kwenda nchi jirani, nenda ukasimamie vizuri” amesema Mhe. Samia.
Amemtaka pia Mhe. Mtambi kuweka mikakati ya kuuinua Mkoa wa Mara kiuchumi kwa kushirikiana kwa ukaribu na Mkoa wa Kagera na kusimamia vizuri mpaka na nchi jirani na rasilimali za nchi ikiwemo Ziwa Victoria, Mto Mara na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Rais Samia alimteua Mhe. Mtambi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara tarehe 31 Machi, 2024 ambaye amechukua nafasi ya Mhe. Said Mohamed Mtanda ambaye amehamishiwa Mkoa wa Mwanza. Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Mtambi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga.
Katika hafla ya kuwaapisha viongozi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Samia amewaapisha pia viongozi wengine wakiwemo Waziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Mikoa, Manaibu Katibu Wakuu, Jaji wa Mahakama Kuu, viongozi wa Idara ya Mahakama na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa