Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Naano Anney leo amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kwenye mapokezi ya nyumba (6 in one) iliyojengwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali Project Zawadi kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Bukama, Kata ya Nyamuswa Wilaya ya Bunda.
Akizungumza baada ya kuzindua nyumba hiyo, Mhe. Anney amelipongeza Shirika hilo kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba hiyo kwa gharama nafuu na pamoja na miundombinu mingine katika shule hiyo yenye lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Nyumba hii ni kubwa yenye uwezo wa kuchukua familia sita lakini imejengwa kwa gharama nafuu kwa ubora na viwango vizuri, kama Serikali tuna la kujifunza hapa katika ujenzi huu” amesema Mhe. Dkt. Anney.
Mheshimiwa Anney pia ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi waliochangia nguvu zao kuleta viashiria vya ujenzi katika mradi huo na kuwataka wananchi wote kushiriki shughuli za maendeleo ya kijiji hicho pale inapohitajika.
Amewataka walimu watakaopewa nyumba hizo kuzitunza ili ziendelee kuwa kwenye ubora wake na kudumu muda mrefu ili kupunguza tatizo la uhaba wa nyumba za walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kazi iliyofanywa na Shirika la Project Zawadi ni kubwa, imeacha alama kwa wananchi na Serikali na imeunga mkono juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na hususan katika shule za Msingi na Sekondari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Amos Mbilinyi amesema kuwa Halmashauri hiyo kwa sasa inamahaitaji ya nyumba zaidi ya 854 za walimu na mpaka sasa ina nyumba 317 na bado inahitaji nyumba zaidi ya 500 ili kuwawezesha walimu kuishi mazingira ya shule.
Bwana Mbilinyi amesema kwa kukabidhiwa nyumba hiyo yenye uwezo wa kuchukua familia sita za walimu, imepunguza tatizo la nyumba kwa walimu hao ambao hapo awali walikuwa wanapanga katika nyumba za watu mbali na eneo hilo la shule.
Bwana Mbilinyi amelipongeza Shirika hilo kwa kuweka mita tofauti za maji na umeme kwenye kila sehemu ya nyumba ili kila mwalimu alipe bili zake kwa kadili ya matumizi yake jambo ambalo litapunguza migogoro baina ya walimu wanaoishi katika nyumba hiyo.
Wakati huo huo, Shirika la Project Zawadi leo limekabidhi kompyuta mpakato (laptops) mbili kwa Watendaji wa Kata za Nyamuswa na Salama ikiwa ni mwendelezo wa shirika hilo kuwawezesha vitendea kazi watumishi wa Serikali wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Waliokabidhiwa kopmyuta hizo na Mkuu wa Wilaya ya Bunda ni Bwana Hanington Teikwa Mugabe Mtendaji wa Kata ya Nyamuswa na Bwana Reuben Maduhu wa Kata ya Salama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bukama Bwana Riganya M. Riganya amelishukuru Shirika la Project Zawadi kwa kufanya miradi mingi katika shule hiyo ikiwemo ujenzi wa vyoo, ukarabati wa madarasa na kuweka mfumo wa kuvuna maji ya mvua.
Aidha, amesema Shirika hilo limekuwa likitoa mafunzo ya kilimo kwa wanafunzi na wananchi ili waweze kulima chakula na wanafunzi wapate chakula wakiwa shuleni na kuahidi kusimamia utoaji wa chakula shuleni kulingana na mpango wa Kijiji waliouweka.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Project Zawadi Bi. Regina Mkama amesema nyumba hizo zimejengwa kwa gharama ya shilingi 176,192,732 ambapo kati ya fedha hizo wananchi walichangia nguvu kazi yenye thamani ya shilingi 14, 580,000 na shirika hilo lilitoa shilingi 161,612,736.
Bi. Mkama amesema nyumba hiyo ilianza kujengwa mwaka 2021 na imechelewa kukamilika kutokana na wananchi wa Kijiji cha Bukama kusuasua kujitolea katika shughuli za mradi huo kinyume cha sera za Shirika hilo ambapo ni lazima wananchi wachangie katika miradi ya maendeleo na hususan nguvu kazi.
Bi Mkama amesema shirika hilo lenye makao yake makuu Jijini Arusha lilisajiriwa mwaka 2017 na kwa Mkoa wa Mara linatekeleza miradi yake katika Tarafa ya Chamriho, ambapo linahudumia shule 46 za msingi na Sekondari zilizopo katika Kata saba.
Bi. Mkama amesema kwa sasa Shirika hilo linajihusisha na mafunzo kazini kwa walimu, ufadhili wa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu na kuboresha miundombinu ya shule.
Ufadhili wa nyumba ya walimu ni mwendelezo wa miradi ya miundombinu ya elimu zikiwemo nyumba za walimu zilizojengwa na Shirika hilo katika Tarafa ya Chamriho, Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa