Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula amewapongeza watumishi wote wa sekta ya Afya wa Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri wanayoifanya hususan katika udhibiti wa janga la Corona.
Bibi Mthapula ameeleza hayo leo tarehe 25 Julai 2020 katika mji wa Tarime wakati akifunga mafunzo ya timu ya usimamizi wa huduma za afya katika Mkoa wa Mara yaliyotolewa kwa ushirikiano na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) Boresha Afya.
“Pamoja na Mkoa wetu kuwa mpakani lakini kutokana na kazi kubwa mliyoifanya, Mkoa wa Mara hatukupata kabisa wagonjwa kutokea nchi jirani ambazo nyingi zimeathirika zaidi.
Hata hivyo amewataka wataalamu wa afya kuendelea kuhamasisha kuhusiana na tahadhari za kujikinga na Corona kwani watu wameanza kuacha kuchukua tahadhari.
Aidha amewapongeza wataalamu wa afya kwa usimamizi wa ujenzi wa hospitali na vituo vya afya katika Mkoa wa Mara ambavyo vimejengwa katika Mkoa wa Mara katika kipindi hiki cha awamu ya tano.
“Ninawaomba wale ambao wanavituo au hospitali ambazo hazijaanza kutoa huduma waanze mapema iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa” alisema Bibi Mthapula.
Aidha amewataka wataalamu hao kujiandaa na kuziba pengo litakalobakia baada ya mradi huo Boresha Afya kukamilisha shughuli zake mwaka 2021.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga amemshukuru Katibu Tawala kwa kuweza kuhudhuria sehemu ya mafunzo hayo pamoja na kuyafunga rasmi.
Aidha amewataka Waganga wa Halmashauri kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa vituo vya afya na hospitali kama walivyoahidi ili kuweza kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
“Hamna maana kwa serikali kutoa fedha kujenga vituo hivi kama wananchi hawapati huduma za afya kama ilivyokusudiwa” alisema Dkt. Tinuga.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa