Polisi Kanda Maalum ya Tarime/ Rorya imekamata magunia 67 ya madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 3,350 katika Kijiji cha Nyamwigura, Kata ya Binagi, Tarafa ya Inchage Wilaya ya Tarime tarehe 9 Agosti, 2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi wa Tarime/ Rorya, ACP Geofrey Sarakikya ameeleza kuwa bangi hiyo ilikuwa kwenye lori aina ya fuso yenye namba za usajiri T 597 CFY mali ya Bwana Festo Mmassy, Mkazi wa Arusha.
“Dereva wa gari hilo Bwana Samson Mollel alifanikiwa kutoroka kabla ya kukamatwa na kuwaacha wenzake wawili ndani ya gari hilo ambao walikamatwa na msako mkali unaendelea kuwatafuta wahusika wengine wa kosa hilo” alisema Bwana Sarakikya.
Bwana Sarakikya ameeleza kuwa wahalifu hao waliyaficha magunia hayo ndani ya gari kwa kuyafunika na mikungu ya ndizi mbichi ili yasiweze kuonekana wakati wa ukaguzi na uchunguzi wa awali umebaini kuwa bangi hiyo ilikuwa inasafirishwa kwenda Dar es Salaam.
Kamanda huyo wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/ Rorya ameeleza kuwa watuhumiwa wawili waliokamatwa watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
Wakati huo huo, siku hiyo hiyo katika Kijiji cha Mpakani, Kata ya Sirari katika Wilaya ya Tarime Polisi imekamata mawe mawili yanayodhaniwa kuwa ni ya dhahabu yenye uzito unaokadiriwa kuwa gramu 200 yakiwa yanatoroshwa kwenda nchi Jirani ya Kenya.
Bwana Sarakikya ameeleza kuwa mawe hayo yalikuwa yamefichwa ndani ya gari namba aina ya Land Cruiser Prado, rangi nyeusi yenye namba za usajiri KDH 718 T inayomilikiwa na mtu anayesadikiwa ni Raia wa Kenya anayefahamika kwa jina moja la Matiko.
Kwa mujibu wa Bwana Sarakikya, tayari watuhumiwa wawili wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
Mkoa wa Kipolisi (Kanda Maalum ya) Tarime/ Rorya una jumla ya Wilaya za Kipolisi sita ambazo ni Tarime, Sirari, Nyamwaga, Kinesi, Shirati na Rorya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa