Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda leo amewaongoza watanzania katika kumbukumbu ya miaka 100 ya tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Uwanja wa Mwenge, wilayani Butiama.
Mheshimiwa Pinda ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa katika maadhimisho hayo amewataka watanzania kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
“Mwalimu Nyerere kama walivyo Marais wengine wote wa Tanzania alifanya mambo mengi sana mazuri na yenye manufaa kwa Taifa letu, hivyo nitoe wito kwenu tuendelee kumuenzi” alisema Mheshimiwa Pinda.
Mheshimiwa Pinda amewataka Watanzania kufanyakazi kwa bidii na kufuata misingi aliyoiacha ikiwemo amani, umoja, upendo, mshikamano, uadilifu na uzalendo kwa Taifa.
Kwa upande wake, Chifu wa Kabila la Wazanaki na Kiongozi wa Familia ya Mwalimu Nyerere, Chifu Japhet Wanzagi ameiomba Serikali kukamilisha uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinachoanzishwa katika Wilaya ya Butiama.
“Sisi kama familia tunatamani sana, Mama Maria Nyerere naye anatamani kuona wanafunzi wa Chuo hiki wawe wameanza kusoma hapo kabla yeye hajafa” alisema Chifu Wanzagi.
Chifu Wanzagi ameeleza kuwa familia ya Mwalimu Nyerere inaridhika na jinsi Tanzania na dunia kwa ujumla inavyomkumbuka na kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hata baada ya kifo chake.
Chifu Wanzagi ameiomba Serikali kujenga barabara ya kwenda kwenye mashamba ya Mwalimu Nyerere ili vijana na watanzania ambao wangependa kujifunza maisha ya Mwalimu Nyerere waweze kuyatembelea mashamba bila usumbufu.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameishukuru Serikali kwa kuanzisha maadhimisho hay ana kukubali yafanyike katika Mkoa wa Mara.
Aidha Mheshimiwa Hapi ameishukuru sana Serikali ya Awamu ya sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa hivi tunatarajia mambo yakienda vizuri, Uwanja wa Ndege wa Musoma utaanza kutumika kuanzia Desemba, 2022 na ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) zitaanza kutua tena Musoma kama ilivyokuwa awali” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kuanza kutua kwa ndege hizo kutaongeza idadi ya wataalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuinua maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na mikoa ya Jirani.
Mwalimu Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili, 1922 katika Kijiji cha Butiama katika iliyokuwa Wilaya ya Musoma kwa wakati huo ambapo kwa sasa ni Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa