Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za fedha kuongeza mikopo kwa kwa wakulima ili kuboresha uzalishaji wa wakulima hapa nchini.
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameeleza hayo wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa maonyesho ya sikikuu ya wakulima (NANENANE) ambayo kitaifa imefanyika katika viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
“Mikopo itawasaidia wakulima wetu hapa nchini kuongeza tija katika shughuli zao na hivyo kuongeza kipato cha wakulima na taifa kwa ujumla” alisema Mheshimiwa Samia.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Samia kwa sasa taasisi za fedha zinatoa mikopo kwa wakulima kwa asilimia tisa tu jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa mikopo kwa wakulima hapa nchini.
Aidha Mheshimiwa Samia amesema serikali imesimamia uimarishaji wa mnyororo wa thamani ili kuongeza tija kwa wakulima wote hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameishukuru sana serikali kwa kukubali maonyesho haya kufanyika katika Kanda ya Ziwa Mashariki kwa miaka mitatu mfululizo.
“Tunaishukuru sana serikali kwa kukubali kufanya maonyesho haya katika viwanja hivi kwa miaka mitatu mfululizo na yamekuwa na hamasa kwa wakulima wetu hapa nchini” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa imejipanga kubadili shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija zaidi kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli hizo.
Maonyesho ya 28 ya sherehe za wakulima (NANENANE) yamezinduliwa leo tarehe 1 Agosti 2020 na yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 8 Agosti 2020 Kauli mbiu ya maonyesho ya NANENANE mwaka huu ni kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua kiongozi Bora 2020.
Kwa upande wa maonyesho ya viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu yameandaliwa na Kanda ya Ziwa Mashariki ambayo inahusisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa