Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko leo amewaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara.
Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Dkt. Biteko amesema Jenerali Musuguri ametoa sehemu kubwa ya maisha yake kuhakikisha Tanzania inakuwa na amani, usalama na mshikamano wa kitaifa na kuwataka watu wote kuiga mfano wake na kujiuliza ni jambo gani wao kama wananchi wa Tanzania watakumbukwa nalo.
“Katika uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo? Huyu ameacha alama ya uzalendo, kujitoa kwake kuipenda nchi---- alikuwa mstari wa mbele kuliokoa taifa lake, tujiulize sisi tuliobakia tutaacha alama gani” amesema Mhe. Dkt. Biteko.
Mhe. Dkt. Biteko amewataka Watanzania kumuenzi Jenerali Musuguri kwa kuilinda amani na utulivu wa Nchi yetu na hasa katika kipindi hiki nchi inapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 na kuongeza kuwa bila amani na utulivu hamna maendeleo yanayoweza kupatikana.
Dkt. Biteko amesema Jenerali Musuguri wakati wote akiwa Jeshini alikuwa mstari wa mbele katika kuliokoa Taifa na kuongeza kuwa Serikali daima itauenzi mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa uhai wake kwa kuendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na amani na utulivu.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Kizanaki, Chifu wa Kabila la Wazanaki, na Kiongozi wa familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Chifu Japhet Wanzagi amesema wananchi wa Butiama na Watanzania tumeondokewa na mtu muhimu sana aliyekuwa na karama, uwezo na kipaji cha ajabu na kumwelezea marehemu Musuguri kuwa alikuwa mpenda watu, mnyenyekevu aliyemjali na kumthamini kila mtu.
“Huyu hakuwa na ukwasi wa mali bali tajiri wa utu wema, watu wengi tulipenda kukaa nae na kuzungumza nae mara kwa mara, alikuwa ni mkarimu na mwenye moyo wa kuwasaidia wahitaji na kuzivaa shida zao” amesema Chifu Wanzagi.
Chifu Wanzagi amesema marehemu alikuwa anauwezo wa kuongea lugha nyingi za makabila ya Afrika Mashariki na hivyo watu wengi walipenda kumsikiliza akiongea kwa kuwa alikuwa anazifahamu na kuziongea lugha zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda amesema kifo cha Jenerali Musuguri ni msiba mkubwa kwa Tanzania na Jeshi la Wananchi wa Tanzania litaendelea kuuenzi mchango wake katika kuanzishwa kwa jeshi hilo na mazuri yote aliyofanyanya wakati alipolitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 45.
“Alishiriki vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilimjenga, kumkomaza na kumpa uzoefu mkubwa na aliporejea nchini aliutumia uzoefu huo kwa ajili ya kujenga nchi yake na kuandaa mipango mbalimbali ya kivita ambayo nchi yetu ilishiriki ikiwemo Vita vya Kagera na vita vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika” amesema Jenerali Mkunda.
Jenerali Mkunda amesema Tanzania itaendelea kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika Vita vya Kagera na pamoja na shughuli mbalimbali za kijeshi zilizofanyika hapa nchini na nje ya Nchi ya Tanzania kwa nyakati tofauti tofauti.
Jenerali Mkunda amemtaja Jenerali Musuguri kuwa wakati wa uhai wake na hususan akiwa jeshini alikuwa shupavu, hodari, shujaa na Jenerali aliyewapenda sana askari wake.
Akitoa mahubiri wakati wa misa ya mazishi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amesema marehemu Musuguri katika uhai wake alikuwa anawaunganisha watu wa makundi yote na ndio sababu ya watu wengi kujitokeza kwa ajili ya kumuaga na kumsindikiza katika mazishi yake.
Mhashamu Askofu Msonganzila amesema Mungu aliwaumba binadamu ili wamjue, wampende, wamtumikie na mwisho waende kwake mbinguni na hivyo Jenerali Musuguri yeye ameianza hiyo safari ya kwenda mbinguni akiwa ameacha alama kubwa hapa duniani.
Askofu Msonganzila amewataka waombolezaji kuendelea kumuombea Jenerali Musuguri na kujiombea wao wenyewe kwa kuwa kwa mujibu wa imani, Yesu alikufa, akazikwa na akafufuka na Mungu atawakutanisha wote waliofariki wakimwamini na Yesu Kristu.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara na baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, viongozi wa Chama cha Mapinduzi na viongozi wa taasisi za umma na binafsi.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Wakuu wa Jeshi la Ulinzi Wastaafu, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Ndugu Philemon Luhanjo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro Nyerere, wakuu wa vyombo vya ulinzi wastaafu na baadhi ya maafisa na watumishi wa umma wa Mkoa wa Mara wameshiriki mazishi hayo.
Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alizaliwa tarehe 4 Januari, 1920 katika Kijiji cha Butiama na kufariki tarehe 29 Oktoba, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo Mwanza na leo amezikwa kwa heshima za kijeshi na kupigiwa mizinga ya heshima 17 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa