Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Wilson Charles Mahera ameanza ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Mara tarehe 3 Juni, 2023 kwa kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda na Hospitali ya Manyamanyama iliyopo katika Mji wa Bunda.
Akizungumza katika ukaguzi na vikao na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda, Dkt. Mahera amemuagiza Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya Ukaguzi wa Ndani kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
“Ninatoa wiki mbili taarifa ya ukaguzi wa ndani ya hospitali hii ifike mezani kwangu ili kujiridhisha kuhusu matumizi ya fedha za ujenzi wa hospitali hii na hususan zilizoletwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi huu” alisema Dkt. Mahera.
Dkt. Mahera ameeleza kuwa taarifa ya ukaguzi wa ujenzi wa hospitali hiyo itatoa mwanga kwa yaliyokuwa yamejiri wakati wa ujenzi ili kama kulikuwa na ubadhilifu au ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma wahusika waweze kufuatiliwa na Serikali.
Aidha, Dkt. Mahera amemuagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda kuendelea kufuatilia kwa ukaribu kesi ya wizi wa vifaa vya hospitali iliyopo Polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kurejesha vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 56.
Dkt. Mahera amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kufanya usimamizi wa karibu zaidi katika ujenzi wa hospitali hiyo ili kurekebisha mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo.
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI ameagiza pia kufufuliwa kwa kamati za ujenzi wa hospitali hiyo kulingana na mwongozo wa force account ili kuendelea kusimamia mradi huo kama ilivyokuwa awali kabla hazijaacha kufanyakazi ya usimamizi.
Wakati huo huo, Dkt. Mahera na timu aliyoambatana nayo wamepongeza ubora wa majengo yaliyojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda pamoja na ujazaji wa taarifa za masuala ya chanjo katika hospitali hiyo.
Wakati huo huo, Dkt. Mahera amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha wanafunga mfumo wa kukusanyia mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya wa GOTHOMIS katika vituo vyote vya Serikali ili kudhibiti upotevu wa mapato katika vituo hiyo.
“Kila kituo cha kutolea huduma za afya kiwe na angalau kompyuta sita na kifungwe mfumo wa GOtHOMIS ifikapo tarehe 30 Juni, 2023 ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Halmashauri” amesema Dkt. Mahera.
Katika Hospitali ya Mji wa Bunda Dkt. Mahera ameipongeza Halmashauri hiyo kwa ujenzi wa majengo matatu yaliyo katika hatua mbalimbali na kuitaka Halmashauri kufuata mwongozo wa force account katika utekelezaji wa ujenzi huo.
Katika Hospitali ya Manyamanyama Dkt. Mahera amezungumza na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya inayofanya ukaguzi na uwajengea uwezo watumishi katika hospitali hiyo ili kupata mrejesho wa mambo waliyoyabaini katika uwepo wao katika Mkoa wa Mara katika kipindi cha wiki tatu walizokaa katika Hospitali hiyo na Kituo cha Afya Nyasho kilichopo katika Manispaa ya Musoma.
Ratiba ya viongozi hao inaonyesha kuwa tarehe 4 Juni, 2023 Dkt. Mahera anaendelea na ziara yake kukagua miundombinu ya afya inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Mji wa Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mahera aliongozana na wataalamu wengine wanne kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa