MZEE AWATAKA WALIMU KUWA WABUNIFU
Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewataka walimu wa shule mbalimbali katika Mkoa wa Mara kuwa wabunifu na kujiongeza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Mzee ametoa wito huo wakati akifanya ziara ya kupokea vyumba vya madarasa katika Wilaya ya Serengeti na kuwaelekeza walimu kuanzisha miradi mbalimbali ya kuongeza mapato ya shule ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Walimu wetu hawana ubunifu, wa kujiongezea au kufanya mabadiliko katika shule zetu, Shule zinaweza kufanya biashara ndogo ndogo na kupata pesa za kuweza kutatua changamoto ndogo ndogo zinazowakabili” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa miradi itakayoanzishwa inaweza kutoa huduma na elimu kwa vitendo kwa walimu na wanafunzi wanaosoma katika shule hizo na wananchi wanaowazunguka maeneo ya shule.
Aidha, amewataka walimu kutumia fursa ya kuwa na wanafunzi wengi kubuni miradi ambayo itawasaidia kupata fedha za kutatua changamoto mbalimbali pindi zinapojitokeza.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka walimu na wasimamizi wa elimu kusimamia suala la uboreshaji wa mazingira ya shule kwa kupanda miti, maua, matunda na kuyasawazisha maeneo ya shule na kuzuia mmomonyoko wa udongo katika shule zao ili wanafunzi waweze kupita vizuri.
“Mazingira yanatakiwa yawe mazuri ili wanafunzi wapende kwenda shule na wakienda wajifunze kitu kutokana na ubunifu katika kuongeza mapato na kutunza mazingira” alisema Mheshimiwa Mzee.
Katika ziara hiyo, kati ya shule tano alizotembelea, Shule ya Sekondari Rigicha pekee ilitoa taarifa ya kuwa na mradi wa shule wa ufugaji wa nyuki, lakini shule nyingine zilitoa taarifa ya kuwa na mpango wa kuanzisha miradi lakini bado hawajapata mtaji wa biashara.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Katibu Tawala sehemu ya Elimu, Katibu Tawala sehemu ya Miundombinu, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, watumishi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Menejimenti ya Wilaya ya Serengeti na viongozi wa CCM Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa