Mwenge wa Uhuru leo tarehe 26 Julai, 2024 umeanza mbio zake katika Wilaya ya Serengeti ambapo umetipia miradi tisa yenye thamani ya shilingi 6,274,190,935.39 na kugawa vyandarua, kuzungumza na klabu ya wapinga rushwa na kugawa viti vya kuwasaidia kutembea watoto wenye ulemavu wa viungo.
Katika mradi wa bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Robanda, Mwenge wa Uhuru umezindua bweni hilo lenge thamani ya shilingi 220,873,984.00 huku kiongozi wa Mbio za Mwenge Ndugu Godfrey akitoa maelekezo ya kuondoa vitanda vilivyozidi katika bweni hilo kwa ajili ya usalama wa wanafunzi.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umefungua mradi wa maji wa Kata ya Issenye wenye thamani ya shilingi 1,971,903,869.64 na katika mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alitoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya mfumo wa NEST katika manunuzi ya umma.
Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa soko la Kijiji cha Makundusi lililojengwa kwa gharama ya shilingi 122,865,560.00 kutokana na mapato ya kijiji hicho na mchango wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Akiwa katika eneo hilo, Ndugu Mnzava alitoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi waliokuwa wamekusanyika katika mradi huo na kuwaasa kuwachagua viongozi bora na kuwaepuka watu wanaoanzisha uchochezi na vurugu hususan wakati huu Taifa linapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwenge wa Uhuru pia umekagua na kuweka jiwe la msingi katika barabara ya Park Nyigoti –Nyichoka yenye daraja na makalavati 30 yenye thamani ya shilingi 2,147,948,000.00 iliyotolewa na Benki ya Ujerumani (KFW) kupitia Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA).
Aidha, Mwenge wa Uhuru umezindua Zahanati ya Bokore iliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Ujerumani kupitia TANAPA kwa thamani ya shilingi 380,736,450 na kugawa vyandarua 400 kwa baadhi ya wananchi wa eneo hilo, kikundi cha Umoja wa bodaboda cha Morotonga.
Mwenge pia ulitembelea Shule ya Watoto wenye mahitaji maalum na kugawa viti vya kuwasaidia kutembea, ukazindua Chuo cha Ufundi cha World Changer na kutembelea daraja la Tabora B lenye thamani ya shilingi 253,769,071.75 ambalo lilizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kuangalia uendelevu wa mradi.
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru umefanyika katika Uwanja wa Right to Play, Mugumu na baada ya hapo Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na makabidhiano yatafanyika katika Kijiji cha Kerende.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa