Mwenge wa Uhuru unaoendelea na mbio zake katika Mkoa wa Mara umefika nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuwasha mwenge wa asili unaofahamika kama Mwenge wa Mwitongo.
Mwenge wa Mwitongo umewashwa leo tarehe 26 Juni 2021 ikiwa ni sehemu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ambapo kila mwaka Mwenge wa Uhuru hupita nyumbani kwa Baba wa Taifa na kuwasha Mwenge wa Mwitongo kama kumbukumbu ya muasisi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa.
“Mwenge huu umekuwa ukiwashwa miaka yote tangu Baba wa Taifa akiwa hai kila Mwenge wa Uhuru unapofika katika Mkoa wa Mara, ni tukio zuri kwa kweli kulishuhudia” alisema mwananchi baada ya kuwashwa kwa mwenge huo.
Baada ya kuwasha Mwenge wa Mwitongo, viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa walipata nafasi ya kusalimiana na familia ya Nyerere iliyoongozwa na Chifu Japhet Wanzagi Nyerere akiambatana na Mtoto wa Baba wa Taifa Bwana Madaraka Nyerere na wanafamilia wengine.
Aidha viongozi hao walitumia fursa hiyo kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere na wakiwa hapo waliweka mashada ya maua na kuwasha mishumaa.
Akiwa nyumbani kwa Baba wa Taifa pia, kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa alikabidhi pikipiki kwa kikundi cha vijana, kukagua mradi wa kikundi cha wanawake, kufungua kikundi cha wapinga rushwa na kupatiwa maelezo kuhusu Jukwaa la Mobile Kilimo.
Aidha Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kitaifa akiwa eneo hilo alitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ujumbe wa Mwenge kitaifa kwa mwaka 2021.
Mwenge wa Uhuru unakesha leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyamsisi na kesho unatarajiwa kukabidhiwa katika Wilaya ya Bunda ili kukamilisha mbio zake katika Mkoa wa Mara.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu tarehe 28 Juni 2021 asubuhi kuendelea na mbio zake mkoani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa