Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongela katika viwanja vya Shule ya Msingi Robanda, Wilaya ya Serengeti.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mhe. Mtanda ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umejiandaa vizuri kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri zake tisa ambazo ni Serengeti DC, Butiama DC, Tarime DC, Tarime TC, Rorya DC, Musoma MC, Musoma DC, Bunda TC na Bunda DC na kuukabidhi Mwenge wa Uhuru salama katika Mkoa wa Mwanza tarehe 13 Julai, 2023.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa kama ilivyo kawaida ya miaka yote Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Mara utawasha Mwenge wa Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Wilaya ya Butiama.
“Hili ni tukio kubwa na la kihistoria katika Mkoa wetu na ninawakaribisha sana kutembelea na kuweka mashada ya maua katika Kaburi na Kutembelea makumbusho ya Baba wa Taifa mkiwa katika Wilaya ya Butiama” amesema Mhe. Mtanda.
Wakati huo huo, Mhe. Mtanda ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Mara utakimbizwa katika jumla ya kilomita 1097 na utapita katika miradi ya maendeleo 63 yenye thamani ya shilingi bilioni 17.
“Miradi inayopitiwa na Mwenge wa Uhuru ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, ustawi wa jamii, viwanda na biashara” ameeleza Mhe. Mtanda na kufafanua kuwa miradi hiyo imegharimiwa namichango ya wananchi wa Mkoa wa Mara, Halmashauri, Serikali Kuu na wahisani wa maendeleo.
Aidha, Mhe. Mtanda amempongeza Mhe. Mongela kwa kuhitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru salama na kuwatunza vizuri wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wakati wote walipokuwa katika Mkoa wa Arusha.
Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yamehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini.
Wengine waliohudhuria ni Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, viongozi wa mila, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa