Mwenge wa Uhuru leo tarehe 27 Juni 2021 umekamilisha mbio zake katika Mkoa wa Mara kwa kuhitimisha mbio zake katika Wilaya ya Bunda.
Kwa sasa Mwenge wa Uhuru leo ikiwa ni siku ya mwisho kuwa Mkoani Mara unaendelea na mkesha unaofanyika katika Chuo cha Ualimu Bunda.
Akizungumza baada ya chakula cha jioni Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Maalum mwaka 2021 Lt. Josephine Paul Mwambashi ameshukuru kwa mapokezi na ushirikiano walioupata wakiwa katika Mkoa wa Mara.
“Tumepata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wananchi ambao umerahisisha ukaguzi wa miradi na mbio za mwenge kwenda vizuri bila tatizo lolote” alisema Mwambashi.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Bunda, umepokelewa katika stendi ya mabasi ya Nyamswa na baada ya hapo ukatembelea mradi wa ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya (GOTHOMIS) katika Kituo cha Afya Ikizu na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari ya Hunyari.
Aidha Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa maji wa Kihumbu na umetembelea na kukagua Jukwaa la kielektroniki wa utoaji wa huduma za ugani na masoko kwa wakulima (M-Kilimo) na mfumo wa malipo ya mauzo ya pamba kwa njia ya kielektroniki.
Mwenge wa uhuru pia umeweka jiwe la msingi katika mradi wa Zahanati ya Mary Imaculate uliopo katika eneo la Bunda Stoo, umetembelea mradi wa ujasiliamali wa vijana wa utengenezaji mapambo na mikoba, umezindua mradi wa kiwanda cha tofali cha Halmashauri ya Mji wa Bunda na kutembelea mradi wa ukarabati wa Chuo cha Ualimu Bunda.
Kesho tarehe 28 Juni 2021 asubuhi Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu tayari kwa kuendelea na mbio zake mkoani humo.
Mwenge wa Uhuru uliwashwa tarehe 17 Mei 2021 katika Mkoa wa Kusini Unguja na unatarajiwa kukamilisha mbio zake katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita tarehe 14 Oktoba 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa