Mwenge wa Uhuru leo umeanza kukimbizwa katika Mkoa wa Mara kwa kukimbizwa katika Wilaya ya Serengeti ambapo umezindua miradi miwili, kuweka mawe ya misingi katika miradi mitatu, kutembelea kikundi cha vijana cha ufugaji wa kondoo na vilabu vya wapinga rushwa na mazingira.
Miradi iliyozinduliwa ni pamoja na mradi wa daraja la Tabora B linalosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ikiwa ni sehemu ya madaraja matano na mradi wa vyumba vya madarasa viwili, ofisi ya walimu, tenki la maji na vyoo vya wanafunzi katika Shule ya Msingi Kisangula miradi ambayo ni sehemu ya miradi mikubwa inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) katika Wilaya ya Serengeti.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umeweka mawe ya msingi katika mradi wa maji unaosimamiwa na Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (TARURA) katika Kijiji cha Nyibirekera na mradi wa zahanati katika Kijiji cha Nyibirekera ikiwa ni sehemu ya miradi ya ujenzi wa zahanati, nyumba za watumishi na miundombinu ya afya inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha World Changer kinachofadhiliwa na Taasisi moja ya kidini nchini Ujerumani.
Mbali na miradi hii, Mwenge pia umetembelea kikundi cha vijana wanaofuga kondoo na kilichopata mkopo wa Halmashauri katika eneo la Natta na vilabu vya Rushwa na Mazingira katika Shule ya Msingi ya Kisangula.
Akizungumza kuhusiana na miradi ya Wilaya ya Serengeti, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Mhe. Abdalla Shaib Kaim ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru umekagua na kuridhishwa na nyaraka za miradi, ubora na gharama za miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mhe. Kaim ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuwasaidia vijana wanaojihusisha na kikundi cha ufugaji wa kondoo ili kuweza kukua na kufanya uzalishaji ambao utaongeza kipato na ajira kwa wanakikundi na wananchi wengine katika eneo hilo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Serengeti zilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Mbunge wa Serengeti, viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na wananchi wa Wilaya ya Serengeti.
Kesho tarehe 5 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambapo ukiwa hapo unategemewa kuwasha Mwenge wa Mwitongo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa