MWENGE WA UHURU KUPITIA MIRADI YA BILIONI 24.96 MARA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ofisini kwake ametoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 katika Mkoa wa Mara mapokezi yake yanayotarajiwa kufanyika kesho katika uwanja wa Shule ya Msingi Robanda, Wilaya ya Serengeti.
Mhe. Mtambi amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka huu zitapita katika miradi ya maendeleo 72 yenye thamani ya shilingi 24,961,723,115.48 iliyotekelezwa kwa michango ya wananchi, Halmashauri, Serikali Kuu na wahisani.
“Miradi itakayotembelewa ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, mazingira, ustawi wa Jamii, viwanda na biashara na shughuli za vijana” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema maandalizi ya kupokea Mbio za Mwenge wa Uhuru yamekamilika na ukiwa katika Mkoa wa Mara utakimbizwa katika Wilaya sita na Halmashauri tisa katika umbali wa kilomita 1,037.80.
Kanali Mtambi amesema ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni kuhusu utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya kauli mbiu: Tunza Mazingira na shiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu.
Akizungumzia ratiba ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kanali Mtambi amesema Mwenge unatarajiwa kukimbizwa kuanzia Serengeti tarehe 26/ 7/ 2024, Tarime DC tarehe 27/7/2024, Tarime TC tarehe 28/7/2024, Rorya 29/7/2024 na Manispaa ya Musoma tarehe 30/7/2024.
Mwenge utakimbizwa Musoma DC tarehe 31/7/2024, Butiama tarehe 1/8/2024, Bunda DC tarehe 2/8/2024, Bunda TC tarehe 3/8/2024 na tarehe 4/8/ 2024 Mwenge utakabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu kuendelea na mbio zake.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amewakaribisha viongozi, watendaji na wananchi wote kushiriki katika maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Mwitongo yatakayofanyika nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo tarehe 1 Agosti, 2024.
Mwenge wa Mwitongo ni mwenge wa Kabila la Wazanaki ambao upo Nyumbani kwa Baba wa Taifa na unawashwa kila mwaka Mbio za Mwenge wa Uhuru zikiwa katika Mkoa wa Mara tangu mbio hizo zilipoanzishwa mwaka 1964.
Mhe. Mtambi amesema mwaka huu ni mwaka maalum kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo unaadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mhe. Mtambi amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara ambao wamechangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hususan itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wote kushiriki mbio, mapokezi, mikesha na shamrashamra za Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa