Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuingia katika Mkoa wa Mara leo tarehe 22 Juni 2021 ukitokea katika Mkoa wa Arusha na kupokelewa katika Sekondari ya Robanda iliyopo katika Kijiji cha Robanda katika Pori la Akiba la Ikilongo pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Mara, leo baada ya kupokelewa kutoka Mkoa wa Arusha utakimbizwa katika Wilaya ya Serengeti na kesho utakabidhiwa katika Wilaya ya Tarime.
Ukiwa katika Wilaya ya Serengeti, Mwenge wa Uhuru unatarajia kuzindua mradi wa bwalo la chakula na mradi wa maji katika Shule ya Sekondari Robanda; kuweka jiwe la msingi mradi wa lambo la mifugo; kuzindua ofisi ya Kijiji cha Park Nyigoti; kufungua mradi wa zahanati ya kijiji cha Koreri; pamoja na kutembelea kitalu cha miche na kuzindua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa katika Shule ya Sekondari ya Kitunguruma.
Aidha Mwenge wa Uhuru unatarajia kufungua Kituo cha Polisi stendi mpya ya Mugumu; Kukagua mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya hospitali (GOTHOMIS) katika Hospitali ya Nyerere (DDH); kutembelea mradi wa barabara ya lami na kukagua shughuli za vijana zinazofanywa na kikundi cha Bloom Youth Group mjini Mgumu.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mkesha wa Mwenye wa Uhuru utafanyika katika Stendi ya Zamani mjini Mugumu ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwepo na burudani mbalimbali.
Kauli mbiu ya mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu “TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu: Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 17 Mei 2021 katika Mkoa wa Kusini Unguja na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana Kitaifa 2021 itafanyika mkoani Geita tarehe 14 Oktoba 2021.
Katika Mkoa wa Mara Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kuanzia leo hadi tarehe 27 Juni 2021 na tarehe 28 Juni 2021 utakabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa