Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula amewataka wanawake wa Manispaa ya Musoma kuchangamkia mikopo ya wanawake inayotolewa na halmashauri yenye lengo la kuwakomboa kiuchumi.
Mama Mthapula ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Machi 2021 alipokuwa Mgeni Rasmi katika kongamano la Siku ya Wanawake Duniani katika Manispaa ya Musoma lililofanyika katika Ukumbi wa MCC uliopo ndani ya eneo la Chuo Kikuu Huria, katika mji wa Musoma.
“Tunaishukuru sana serikali kwa kutenga asilimia nne ya mapato ya ndani kutolewa kama mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake waliojiunga katika vikundi vya uzalishajimali na ujasiriamali” alisema Bibi Mthapula.
Mheshimiwa Mthapula ameeleza kuwa mikopo hiyo ambayo inatolewa kama sehemu ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mujibu wa sheria haina riba yoyote, wanawake wanatakiwa kuichukua na kurejesha mapema ili wenzao pia waje wakope.
Aidha ametoa wito kwa wanawake kushiriki katika malezi bora ya watoto katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo na kushirikisha wanawake wa aina tofauti tofauti katika kongamano hilo.
Kwa Upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa Patrick William Gumbo amewataka wanawake kupendana na kusaidiana katika kufikia malengo yao.
“Ninaomba kuwasihi wanawake msaidiane na mwanamke mmoja akipanda awe daraja la kuwavusha wananwake wengine waweze kupanda pia” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Ameeleza kuwa haki ya wananwake ipo lakini wanahitaji kuitafuta hawataipata bila mapambano na katika mapambano hayo ushirikiano wa wao kwa wao ni muhimu sana.
Ameeleza kuwa katika Mkoa wa Mara kuna Katibu Tawala mwanamke, wakuu wa wilaya wawili wananwake na wakurugenzi wa halmashauri watatu ni wananwake, wakitumika vizuri wanaweza kuwavusha wanawake wengi zaidi kupata nafasi za uongozi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Msoma Bibi Fidelica Myovella ameeleza amewahimiza wanawake kuchangamkia mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri ili kuinua hali yao ya kiuchumi.
Bibi Myovella ameeleza kuwa katika Manispaa ya Musoma kuanzia mwaka 2018/2019 hadi Desemba 2020 vikundi vya wanawake 150 na wanafuika 660 wamepata mkopo unaotolewa na Manispaa kwa ajili ya wananwake.
Aidha Bibi Myovella ameeleza kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake Manispaa ya Musoma yalianza tarehe 7 Machi 2021 ambapo manispaa iliandaa bonanza la michezo kwa ajili ya waheshimiwa madiwani na washindi wa bonanza hilo walipata zawadi.
Kauli mbiu ya siku ya wananwake duniani mwaka huu ni Wanawake katika Uongozi, Chachu ya kufikia Dunia yenye Usawa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa