Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameshiriki msiba wa Mwandu Malegesi mmoja kati ya waendesha pikipiki (bodaboda) wanne waliouawa katika Wilaya ya Butiama na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia tarehe 27 Mei, 2023 na kuwataka wananchi kutulia wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi .
Akizungumza katika msiba huo na katika kijiwe cha bodaboda katika Kitongoji cha Kuoko, Kijiji cha Nyamikoma Wilaya ya Butiama Mhe. Mtanda amewataka wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wakati linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Tutapambana na jambo hili hadi wanaohusika wakamatwe ili matukio ya namna hii yasijitokeze tena katika Wilaya ya Butiama na Mkoa wa Mara” amesema Mheshimiwa Mtanda.
Mheshimiwa Mtanda ametoa pole kwa wafiwa wote na kukemea vikali mauaji yaliyotokea katika Wilaya ya Butiama na kuahidi kushirikiana na wananchi kutokomeza vitendo hivyo.
“Mimi nina wajibu kusimamia usalama wenu na wananchi wote wa Mkoa wa Mara ……kama Serikali tunafahamu umuhimu wa usalama katika shughuli za usafirishaji mnazofanya na tunalichukua jambo hili kwa uzito unaostahili lakini tunaomba ushirikiano ili iwe rahisi kuwabaini wahusika” amesema Mhe. Mtanda.
Amewahakikishia waendesha bodaboda kuwa “Mimi pamoja na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara tutafanya uchunguzi wa kina kwa sababu tukio hili ni mara ya tatu sasa linajirudia katika eneo hili” amesema Mhe. Mtanda.
Katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa amepokea kero mbalimbali za wananchi na bodaboda hao na kuzitolea ufafanuzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa