Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amezungumza na wananchi wa Kata ya Nyarukoba, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kutaka fedha ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) inayotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kugawanywa kwa mujibu wa Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za Mwaka 2023.
Akizungumza na wananchi hao katika uwanja wa Shule ya Sekondari Bwirege, Mheshimiwa Mtanda ameeleza kuwa Kanuni hizo zinazotokana na Sheria ya Madini zinatoa mgawanyo wa makusanyo ya CSR kwa vijiji na Halmashauri ambayo inachimbwa madini na kuziwezesha Halmashauri nzima kunufaika kutokana na uwepo wa migodi katika maeneo yao.
“Kwa mujibu wa Kanuni hizo asilimia 40 ya mapato ya CSR yatatumika katika miradi ya kijiji au mtaa ambapo shughuli za madini zinafanyika na asilimia 60 kwa ajili ya miradi ya Halmashauri ambako shughuli za madini zinafanyika” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda pia ameeleza kuwa kwa mujibu wa kanuni hizo, Kamati ya Wataalam inayoongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri kama Mwenyekiti na Katibu wake kuwa Afisa Mipango na wajumbe wengine ni Afisa wa Tume ya Madini, Wawakilishi wawili wa mmiliki wa leseni , Mhandisi, Wakili wa Serikali, Afisa Mazingira, Afisa Maendeleo na Afisa kutokakatika mradi mahususi unaotekelewa na mpango husika.
Kwa mujibu wa Mhe. Mtanda, utekelezaji wa Kanuni hizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime utasaidia katika kupeleka maendeleo kwa Halmashauri nzima ya Tarime tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kanuni hizo ambapo vijiji 11 tu vilivyokuwa vinauzunguka mgodi vilikuwa vinanufaika.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mtanda amewaahidi wachimbaji madini wanaouzunguka Mgodi wa North Mara kupata fursa ya kutumia mtambo wa uchorongaji madini kufanya utafiti katika maeneo yao na hivyo kuwezesha uwekezaji katika maeneo ambayo yana uwezekano wa kupata madini.
“Kwa kutumia mtambo huu, Serikali ya Mkoa itafanya utaratibu wa kuiwezesha North Mara kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha kupima maeneo yao na kuwawezesha kwa utaalamu na ujuzi ili wachimbaji wadogo waweze kunufaika na migodi waliyonayo” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amewataka wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huo kuacha tabia ya uvamizi katika mgodi wa North Mara na kilimo cha bangi badala yake wajielekeze kwenye kutafuta fedha kwa kufanya shughuli halali.
Mhe. Mtanda ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wanaofadhili uvamizi wa mgodi na kilimo cha bangi katika Wilaya ya Tarime kuacha mara moja na Serikali ya Mkoa imeshapata orodha ya wafadhili hao na mkakati wa kuwashughulikia unaandaliwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyarokoba Mhe. Juma Matiko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya mkutano na wananchi wa Kata hiyo na kufuatilia upatikanaji wa umeme katika Kituo cha Afya Genkuru kilichopo katika Kata hiyo.
Mhe. Matiko ameushukuru Mgodi wa North Mara kwa kutoa ajira kwa vijana 40 kutoka katika Kata hiyo wanaolinda katika eneo la mgodi jambo ambalo limeongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa