Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amezindua mradi wa maji wa Bulinga/Busungu uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma unaosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya shilingi bilioni 2.7.
“Huu ni mradi mkubwa sana ambao unawawezesha wananchi kupata maji safi na salama yenye uhakika, rai yangu tuutunze ili udumu ili wananchi wapate manufaa yaliyotegemewa na mradi huu” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameitaka RUWASA kushughulikia kero ya mita za maji zinazolalamikiwa na wananchi na kuwapitia wale wanaolalamika na kuangalia matumizi yao sahihi ya maji ili walipe hiyo wakati RUWASA inajipanga kuwabadilishia mita hizo zinazolalamikiwa.
Aidha, Mheshimiwa Mtanda ameiagiza RUWASA kuanzisha utaratibu maalum wa kusikiliza kero za wananchi kuhusu maji ikiwa ni pamoja kuwatembelea katika vijiji vyao na kusikiliza kero zao kuhudu huduma za maji.
Mhe. Mtanda pia ameiagiza RUWASA kuongeza vituo vya kuchotea maji katika Kijiji cha Busungu na kuitaka RUWASA kuangalia namna ya kuweza kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kuingiza maji majumbani hata kama kwa mkopo utakaorejeshwa taratibu.
Mkuu wa Mkoa pia amewataka wananchi wenye uwezo kuunganisha maji majumbani ili kupata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi na kutumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Musoma Mhandisi Edward Sironga ameeleza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Julai, 2018 na umekamilika Julai, 2021 kwa ufadhili wa Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) na utawanufaisha wakazi 16, 443 kutoka vijiji vitano vya eneo hilo.
Mhandisi Sironga amevitaja vijiji vitakavyonufaika kuwa ni pamoja na Bulinga, Bujaga, Busungu, Bukima na Kikwerege vilivyopo katika Kata za Bulinga, Bukima na Rusoli na kutokana na uwingi wa maji mradi huu unapanuliwa nkuelekea Kata ya Bwasi ambapo wakazi wapatao 12,072 watahudumiwa.
“Mahitaji ya maji kwa wakazi wanaohudumiwa na mradi ni lita 411,075 kwa siku wakati chanzo cha maji cha mradi huo kinauwezo wa kutoa lita 1,344,000 kwa siku ambayo ni sawa na mara tatu na nusu ya mahitaji ya wananchi” amesema Mhandisi Sironga.
Bwana Sironga ameeleza kuwa mradi huo umejenga matenki mawili ya maji, mtandao wa mabomba ya maji yenye urefu wa kilomita 28.11 na majengo mawili kwa ajili ya ofisi ya jumuiya ya watumia maji (BULISUMAKWI).
Aidha, Bwana Sironga ameeleza kuwa pamoja na ukubwa wa mradi na wingi wa maji, mradi huo umefanikiwa kuwaunganisha wateja wa majumbani 185 na wengine wanachota maji katika vituo vya kuchotea maji.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameitembelea na kukagua ujenzi wa Sekondari mpya katika Kijiji cha Wanyere na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameielekeza Halmashauri hiyo kuwataka mafundi waongoze kasi ya ujenzi ili shule hiyo iweze kuanza kuchukua wanafunzi kuanzia Januari, 2024.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka (Mkuu wa Wilaya ya Rorya), Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Musoma Vijijini, watendaji na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa