Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 21 Novemba, 2023 amezindua kliniki ya kusikiliza kero mbalimbali za ardhi Mkoa wa Mara katika uwanja wa Mkendo, Manispaa ya Musoma na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kutoa kero zao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Mtanda ameeleza kuwa wananchi wakitumia fursa hiyo vizuri wataweza kutatua changamoto zinazowakabili katika masuala ya ardhi.
Mhe. Mtanda pia amewakemea watu wanaofanya usanii katika migogoro ya ardhi na kusubiri kujitokeza wakati wanapokuja viongozi wa kitaifa katika Mkoa wa Mara kutoa kero zao, lakini Serikali ya Mkoa inapotoa fursa hawajitokezi.
“Kama wewe ni kweli una kero, unakaa nayo muda mrefu, tunakuita hapa bure hutokei, unasubiri ziara za viongozi, wewe ni msanii na sisi tunajua namna ya kufanyakazi na wasanii” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameitaka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara kuandaa rejesta ya migogoro ili inapotatuliwa iwe inafahamika kwa watendaji na viongozi wengine wanaokuja baadaye katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule ameeleza kuwa Manispaa ya Musoma inadaiwa fidia na wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kujenga taasisi za umma kama vile shule na vituo vya kutolea huduma za afya.
“Kwa sasa Manispaa inadaiwa shilingi milioni 600 za fidia za ardhi na wananchi mbalimbali na imejipanga kuanza kulipa kwa awamu kuanzia mwaka huu wa fedha” alisema Mhe. Haule.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara, Meya wa Manispaa ya Musoma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Maafisa Ardhi kutoka Manispaa ya Musoma na Ofisi ya Kamishana wa Ardhi Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa