Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 8 Novemba, 2023 ameongoza semina ya walimu na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wanaotarajiwa kustaafu ndani ya miaka mitano na kuwataka watumishi kufanya maandalizi ya kustaafu wakiwa bado kazini.
“Haitapendeza kama mnastaafu na kusubiria pensheni ndio uanze maandalizi wakati huo, lakini maandalizi yakianza sasa, ukistaafu unakitu cha kuendelea kufanya” alisema Mhe. Mtanda.
Akizungumza na walimu hao ambao ni wananchama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mara Mhe. Mtanda amewataka walimu hao kufanya maandalizi ya vitu vyote muhimu wakati wakiwa bado kazini ikiwemo sehemu ya kuishi baada ya kustaafu.
Amewataka watumishi hao kuepukana na matapeli baada ya kupokea pensheni yao na kuacha kuwekeza kwenye miradi mikubwa ambayo hawana utaalamu, taarifa sahihi, wala uzoefu nayo ili kuepuka uwezekano wa kupoteza fedha zao.
Mhe. Mtanda amewataka wastaafu watarajiwa hao kuweka akiba ya fedha taslimu benki itakayowasaidia wakati wamestaafu na wakiwa wanasubiria pensheni yao kutoka ili waweze kujikimu.
Katika semina hiyo, mada mbalimbali kuhusu maandalizi ya kustaafu zilitolewa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSF), Benki ya Biashara ya Walimu, Benki ya CRDB na uzoefu wa walimu wengine waliostaafu.
Semina hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robart Makungu, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu Bwana Dominicus Lusasi na viongozi wa Chama cha Walimu Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa