Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameongoza maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo katika Mkoa wa Mara yamefanyika Nyamswa, Wilaya ya Bunda na kuwataka wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali ili kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mtanda amewataka kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali, taasisi za kifedha na kuwahimiza kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo.
“Serikali inatambua umuhimu wa wanawake katika jamii na kutenga mikopo ya aina mbalimbali kwa ajili yao kupitia mikopo ya Halmashauri, mikopo ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na fursa nyingine zilizopo ili waweze kukuza uchumi wao na wasiwe wategemezi katika jamii” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa mikopo ya Halmashauri iliyokuwa imesimamishwa itaanza kutolewa hivi karibuni baada ya Serikali kukamilisha utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo hiyo na kuzitaka Halmashauri kuendelea kuhifadhi fedha kwa ajili ya mikopo hiyo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kuwataka wamuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Mhe. Mtanda amesema kwa maendeleo yaliyofikiwa katika Mkoa wa Mara chini ya uongozi wa Rais Samia atashangaa kama wanawake wa Mkoa wa Mara hawatamuunga mkono Rais Samia katika uchaguzi ujao ili aendelee kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Mtanda amesema kwa sasa Watanzania na hususan wananchi wa Mkoa wa Mara wameelimishwa kwa vitendo kutokana na mambo mengi yanayofanywa na viongozi wanawake na anaamini jinsia haitakuwa kikwazo tena katika chaguzi zijazo na kuwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa amevitaka vyama vya siasa kuwapitisha wanawake wengi zaidi katika nafasi mbalimbali watakazoomba ili kutoa kigezo cha jinsia ya mtu katika nafasi za uongozi na kuliwezesha taifa kupata viongozi wazuri watakaoleta maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara Bibi Nancy Msafiri ameeleza kuwa maadhimisho haya yanatokana na wanawake kutambuliwa kama sehemu muhimu ya jamii kutokana na uhodari, kujituma na kuwa wabunifu katika mambo mbalimbali.
Bibi Msafiri ameeleza kuwa ameitaka jamii kuwekeza kwa watoto wakike ili kuharakisha maendeleo ya jamii na kutoka mfano wa utendaji wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wanawake waliopo hapa nchini.
Bibi Msafiri amewataka wanawake wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Bibi Neema Ibamba ameeleza kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yameanza mwaka 1975 katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Bibi Ibamba ameeleza kuwa kwa sasa maadhimisho haya yanafanyika katika mikoa yote kila mwaka na kitaifa yanafanyika kila baada ya miaka mitano; na katika Mkoa wa Mara maadhimisho haya yamekuwa yakizunguka katika wilaya mbalimbali ambapo mwaka huu yamefanyika katika wilaya ya Bunda.
Bibi Neema akitoa salamu za wanawake ameiomba Serikali ya Mkoa wa Mara kuunga mkono shughuli za wanawake ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Maadhimisho ya siku ya wanawake yamehudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Bunda, Butiama, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Meya wa Manispaa ya Musoma na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, madiwani, wawakilishi wa Wakurugenzi wa Halmashauri, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri na Taasisi za Serikali zilizopo Mkoa wa Mara.
Wengine waliohudhuria ni viongozi wa vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wa eneo la Nyamswa, Wilaya ya Bunda na kauli mbiu ya maadhimisho haya mwaka huu ni “Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa