Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefanya ziara katika eneo lenye mgogoro mpakani mwa Wilaya za Serengeti na Bunda na kuwataka wananchi wa vijiji vya Mikomariro kilichopo Wilaya ya Bunda na Remng’orori kudumisha amani na usalama wakati Serikali inatafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo linalogombaniwa na wananchi wa vijiji hivyo, Mhe. Mtanda ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya wananchi kuendelea kuhatarisha amani ya eneo hilo wakati Serikali tayari imechukua hatua mbalimbali ili kuendelea kushughulikia mgogoro huo.
“Ninyi wananchi wa Remng’orori na Mikomariro ndio mnauwezo wa kuamua kuumaliza mgogoro huu, hapa hatutafuti mshindi, mshindi hapa ni amani na usalama katika eneo hili, hicho kikiwa ndio kipaumbele chetu, mgogoro huu utaisha” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda pia amezungumza na viongozi wa serikali za vijiji na wazee wa vijiji hivyo na kuwataka kuleta mapendekezo Serikalini ya namna bora ya kumaliza mgogoro huo na kuwaomba viongozi hao kukutana kwenye kikao cha pamoja ili kutoa makubaliano yenye lengo la kumaliza mgogoro huo.
“Kwa sasa ninaomba vigingi vilivyowekwa na Serikali viheshimiwe na wananchi wote na kila mwenye haki yake katika mgogoro huu ataipata haki yake, sio kwa kupigana na kuuana bali kwa kufuata sheria na taratibu” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda amewaonya viongozi , watendaji na wananchi wote wanaoendelea kuuchochea mgogoro huo kuwa Serikali ipo makini na itawachukulia hatua za kisehria wahusika wote wa mgogoro huo.
Aidha, Mhe. Mtanda ameeleza kuwa zoezi la upangaji wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji hivyo limesitishwa hadi hapo suluhu ya kudumu ya mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu itakapopatikana.
Kwa upande wao, viongozi na wazee wa vijiji hivyo wamekubali kukutana kwenye kikao cha pamoja cha kutafuta suluhu ya mgogoro huo katika kikao kitakachohudhuriwa pia na viongozi na watendaji wa Serikali.
Wananchi wa eneo hilo wanagombea eneo lililopo mpakani kati ya Wilaya ya Butiama, Bunda na Serengeti uliodumu kwa muda mrefu hata hivyo kwa siku za hivi karibuni mgogoro upo zaidi kati ya wananchi wa Wilaya za Bunda na Serengeti.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Wakuu wa Wilaya na Kamati za Usalama za Wilaya za Bunda na Serengeti, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Ardhi Mkoa, viongozi na watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Bunda na Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa