Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amewakaribisha viongozi, watendaji na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kushiriki katika mapokezi, mbio na mkesha wa Mwenge wa Uhuru wakati wote utakapokuwa katika Mkoa wa Mara.
Mkuu wa Mkoa amesema hayo leo tarehe 3 Julai, 2023 wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Mara yatakayofanyika kesho katika viwanja vya Shule ya Msingi Robanda, Wilaya ya Serengeti.
“Ninawaomba viongozi, watumishi na wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru lakini pia katika mbio zake na mikesha itakayofanyika katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuanzia kesho hadi tarehe 12 Julai, 2023”amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umejiandaa vizuri kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliojitolea kwa hali na mali.
Mhe. Mtanda amewahakikishia wananchi kuwa katika mapokezi, mbio na mikesha na sehemu zote mwenge utakakopita kutakuwepo na burudani na usalama wa kutosha ili kuwawezesha wananchi kuushangilia Mwenge wa Uhuru kwa amani.
Awali, akizungumza katika kikao cha maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru Mhe. Mtanda amewataka viongozi, wadau na watumishi wote walioalikwa kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru bila kukasa.
Aidha, Mheshimiwa Mtanda ameitaka Kamati ya Maandalizi ya Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Mara kutekeleza majukumu yake kama ilivyopanga na kuhakikisha mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yanafana na kuwa mfano wa kuigwa.
Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa katika Mkoa wa Mara kesho ukitokea Mkoa wa Arusha ambapo utakimbizwa hadi tarehe 12 Julai, 2023 na tarehe 13 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa kwa Mkoa wa Mwanza katika eneo la Nansio, Ukerewe.
Kesho Mwenge wa Uhuru baada ya kupokelewa anza mbio zake kwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na mkesha wa Mwenge wa Uhuru utakauwa katika mji wa Mugumu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa