Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 9 Novemba, 2023 amekutana na wadau wa uvuvi katika Mkoa wa Mara na viongozi wa vyama vya wavuvi na kutuma salamu kwa watu wote wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na uvuvi haramu katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ametoa tahadhari hiyo baada ya kupokea taarifa ya wadau wa Uvuvi Mkoa wa Mara iliyoonyesha uvuvi haramu umeongezeka sana katika Ziwa Victoria hali inayosababisha kukosekana kwa samaki katika ziwa hilo.
“Mkoa wa Mara tumejipanga kudhibiti uvuvi haramu, kwa kuanzia tunakutana na wadau wa uvuvi na kutoa elimu ili baadaye tutakapokukamata usiseme umeonewaa au ulikuwa haujui” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa wavuvi haramu wanaweza kuwa wanapata samaki kwa wakati huo lakini wanaharibu kabisa kizazi cha samaki na hivyo kufanya ziwa lisiwe na samaki wa kutosha na mwishoni kutakuwa hamna samaki kabisa.
Amewaomba wavuvi wote kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuwabaini watumishi wa Serikali wasio waaminifu wanaoshirikiana na wavuvi haramu katika kudhibiti kabisa uvuvi haramu katika Mkoa wa Mara
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka wavuvi kutoa kero zao zote zinazowakabili ili Serikali iweze kuzifanyia kazi amewaahidi wavuvi hao Mkoa wa Mara utaendelea kuratibu vikao kama hivyo ili kupata suluhisho za changamoto zinazowakabili wavuvi.
Akitoa taarifa ya wavuvi, Mwanyekiti wa Umoja wa Wadau wa Wavuvi Mkoa wa Mara na Kanda ya Ukerewe Bwana Matete M. Mgongo ameeleza kuwa wavuvi wanakabiliwa na kero kubwa tatu kuu ambazo ni uvuvi haramu, uharibifu wa nyavu na wizi na unyang’anyi wa samaki wakiwa ziwani.
“Kero hizi zinatufanya wavuvi wengi tuendelee kuwa maskini pamoja na kwamba tunajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kujikwamua kimaisha” amesema Bwana Mgongo.
Bwana Mgongo ameeleza kuwa kwa sasa kuna wimbi kubwa la wavuvi haramu waliopo katika Ziwa Victoria jambo ambalo limepunguza idadi ya samaki katika mwambao wa ziwa na hususan upande wa Tanzania na wamechukua hatua mbalimbali lakini hawajapata ufumbuzi wa kudumu.
“ Kwa sasa ili kupata samaki, sisi wavuvi wa Tanzania tunalazimika kwenda kuwahonga walinzi wa nchi jirani ili tuweze kuvua katika nchi hiyo ili kuweza kupata samaki wa uhakika” amesema Bwana Mgongo.
Akizungumzia kuhusu uharibifu wa vyavu ziwani ameeleza kuwa uharibifu huo unafanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wavuvi wa dagaa wanaotuhumiwa kuharibu nyavu za wavuvi wa Sangara na wameshakaa vikao mara nyingi lakini tatizo hilo bado linaendelea.
Kuhusu unyang’anyi na wizi wa samaki, Bwana Mgongo ameeleza kuwa awali walikuwa wanajua ni watu kutoka nje ya nchi lakini kwa sasa wamebaini baadhi ni watanzania na wengine wameshawahi kukamatwa.
Awali, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inamchango mkubwa sana kwa uchumi wa Taifa na mwaka 2022/2023 sekta ya uvuvi katika Mkoa wa Mara iliingiza shilingi 27,530,903,400/=.
“Serikali kupitia Halmashauri mbalimbali ilipata shilingi 1,42,910,472 kutokana na ushuru wa maegesho, ushuru wa samaki na ada ya leseni “ ameeleza Bwana Makungu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa Mkoa wa Mara una eneo la maji lenye ukubwa wa kilometa za mraba 10,854 na ni shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wanaoishi katika mwambao mwa Ziwa Victoria na una mialo ya uvuvi 127 ambapo kati yake 88 tu ndio inayofanyakazi kwa sasa.
Takwimu zinaonyesha kuwa watu wapatao milioni 4.5 hapa nchini wameajiriwa katika mnyororo mzima wa uvuvi na kwa Mkoa wa Mara wananchi 379,707 wameajiriwa katika mnyororo wa sekta ya uvuvi kutoka katika Wilaya zinazopakana na Ziwa Victoria za Butiama, Bunda, Musoma na Rorya.
Kikao Mkuu wa Mkoa na wadau wa uvuvi Mkoa wa Mara ni mwendelezo wa vikao vya Mkuu wa Mkoa na wadau mbalimbali katika kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa