Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 31 Oktoba, 2023 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuagiza wakaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kuchunguza matumizi ya fedha katika ujenzi wa Kituo cha Afya Machochwe.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo baada ya kukagua na kupokea malalamiko ya viongozi na wananchi kuhusiana na kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 520 na mpaka sasa hamna jengo hata moja lililokamilika.
“Kama kuna aliyehusika kukifanya kituo hiki kisifikie malengo, kwanza tushughulike nae (kumfikisha kwenye vyombo vya sheria) kabla hatujatafuta fedha nyingine….Mkoa wa Mara hautageuzwa tena kuwa shamba la Bibi!” amesema Mhe. Mtanda.
Wakati huo huo, Mhe. Mtanda ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuweza kukamilisha majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) na maabara ili yaanze kutumika kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Mtanda amewapongeza wananchi wa Kata ya Machochwe kwa kutoa mchango wa viashiria na fedha taslimu wakati wa ujenzi wa mradi huo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Dkt. Vincent Mashinji ameeleza kuwa Kamati ya Usalama ya Wilaya ilitembelea mradi huo na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) kufanya uchunguzi wa mradi huo.
“Hilo jalada la uchunguzi mpaka sasa PCCB wanalifanyiakazi….. lakini limechukua muda mrefu sana suala hili kuweza kuhitimishwa” amesema Mhe. Mashinji.
Mhe. Mashinji ameeleza kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo Kamati ya Manunuzi inayowahusisha wananchi haikuhusishwa katika manunuzi ya vifaa vya mradi huo.
Dkt. Mashinji amesema vifaa vyote vilinunuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti bila kufuata mwongozo wa force account na vifaa vya ujenzi vilivyonunuliwa ni vingi kuliko mahitaji ya mradi huo.
Aidha, Mhe. Mashinji ameeleza kuwa baadhi ya vifaa vya mradi huo vitatumika kukamilisha majengo yanayoendelea kujengwa na kuhamishiwa katika miradi mingine kwa utaratibu wa kurudishia fedha.
Awali akitoa taarifa za mradi huo, Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Machochwe ameeleza kuwa kwa sasa fedha iliyobakia ni zaidi ya shilingi milioni 14 na vifaa vya zaidi shilingi milioni 30.
Aidha, taarifa hiyo ilionyesha kuwa Kituo hicho kinahitaji shilingi milioni 151 ili kuweza kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Mara alitembelea pia mradi wa maji wa Kenyamonte, Shule ya Msingi Ikorongo, Shule ya Sekondari ya Morotonga na kuzungumza na wananchi katika Kijiji cha Park Nyigoti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa