Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefungua kikao cha tathmini ya Maendeleo ya Elimu Mkoa wa Mara kinachofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuwataka walimu na wasimamizi wa elimu kuongeza ubunifu na kujiongeza katika utendaji wao wa kazi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Mhe. Mtanda amewataka wasimamizi wa Elimu wa ngazi mbalimbali kufanya ubunifu unaochochea mabadiliko chanya kwa walimu na wanafunzi wanaowasimamia na kuacha alama chanya katika utendaji wao.
“Sio lazima mtu uwe na cheo kikubwa ndio ufanye mabadiliko, unaweza kuwa huna cheo lakini kwa namna unavyochapa kazi na kuongeza ubunifu unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika eneo lako kuliko hata mtu mwenye madaraka makubwa ambaye hana ubunifu” amesema Mhe. Mtanda.
Mkuu wa Mkoa pia amewataka Walimu kujiendeleza kimasomo pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ya kazi.
Mhe. Mtanda amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ambao hawajakamilisha ujenzi wa shule mpya na kuzisajiri kufanyakazi usiku na mchana na kuhakikisha wanasajiri Shule hizo kabla ya tarehe 22 Desemba, 2023 ili ziweze kuanza kuchukua wanafunzi Januari, 2024.
Aidha, amewataka Wakurugenzi, Wasimamizi wa Elimu ngazi mbalimbali kuwasikiliza walimu na kujitahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ambazo utatuzi wake upo katika ngazi yao na hauhitaji fedha.
Mhe. Mtanda amewataka wasimamizi wa Elimu kuweka malengo katika utekelezaji wa majukumu yao na katika maisha yao binafsi na kuisemea vizuri Serikali kwa mambo mazuri inayoyafanya kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo Bwana Makwasa Bulenga amewapongeza wasimamizi wa elimu na walimu wa Mkoa wa Mara kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kufundisha wanafunzi na kuwasimamia walimu.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa mwaka 2022 Mkoa ulipanga kufaulisha kwa asiliamia 100 kwa mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita na mwaka 2023 Mkoa umefaulisha kwa asilimia 100 ukiwa na daraja la nne kwa mwanafunzi mmoja tu na kuongeza kuwa matokeo ya mitihani mingine bado hayajatoka lakini anamatumaini kwa kazi iliyofanyika Mkoa wa Mara utafanya vizuri.
Hata hivyo, Bwana Bulenga amesema kwa upande wa mitihani ya kidato cha nne, pili, darasa la saba na darasa la nne bado juhudi zaidi zinahitajika katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya madarasa hayo.
“Kwa umoja wetu tumepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya elimu ya Mkoa wa Mara japo kuna maboresho zaidi yanahitajika hususan katika shule za msingi na kidato cha kwanza hadi cha nne” amesema Bwana Bulenga.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika Mkoa wa Mara kwa mwaka huu, bado Mkoa una upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi jambo ambalo amesema linaathiri ufundishaji wa wanafunzi katika masomo hayo.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa shule mpya, Bwana Bulenga amesema tayari baadhi ya Halmashauri zimeshakamilisha ujenzi wa shule mpya na kuzisajiri huku baadhi ya Halmashauri zikiendelea na ukamilishaji wa shule hizo.
Kwa upande wake Bwana Edigga Sibora Mkuu wa Shule ya Sekondari Sazira, Halmashauri ya Mji wa Bunda amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufungua kikao hicho cha tathmini na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yalitotolewa.
“Sisi tunaahidi hatutakuangusha katika kuleta mabadiliko katika maeneo yetu ya kazi na katika maisha yetu sisi wenyewe” amesema Bwana Sibora.
Kikao hicho cha siku mbili ambacho Mwenyekiti wake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, kimehudhuliwa na Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wasimamizi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Halmashauri, wadau wa elimu na baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa