Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda amezitaka Halmashauri kuchukua hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu ambao tayari umeathiri mikoa ya jirani inayouzunguka Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha tathmini ya utendaji kazi Mkoa wa Mara kilichofanyika ukumbi wa Uwekezaji na kuhudhuriwa na viongozi wa Wilaya na Menejimenti za Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
“Tayari mikoa yote tunayopakana nayo imesharipoti kuwepo kwa ugonjwa huu, sisi tuchukue hatua mapema ili kudhibiti kusambaa kwa kipindupindu na hususan wakati huu wa mvua, na Halmashauri zitoe uzito kwenye jambo hili” amesema Mhe. Mtanda.
Amezitaka Halmashauri kuhuisha timu za muitikio wa dharura, kuandaa vituo vya matibabu na kuweka dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa na mahitaji mwengine na kuandaa mpango wa dharura wa kukabiliana na mlipuko wa ugongwa huo.
Mhe. Mtanda amezitaka Halmashauri kuendelea kutoa elimu ya afya kwa umma kuhusu usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo na kufanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika maeneo yote.
Mhe. Mtanda amezitaka Halmashauri kufanya ukaguzi wa usafi katika masoko, shule, kwenye minada, kaya na maeneo ya biashara ili kuzuia uwezekani wa kutokea mlipuko.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi, kuchemsha maji yakunywa, kutumia vyoo bora, kuosha matunda na mbogamboga kwa maji safi na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao.
Mhe. Mtanda amewataka Wakuu wa Wilaya na viongozi wa Halmashauri kusimamia zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi na kutoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabroni Masatu amesema kwa sasa Mkoa wa Mara hauna wagonjwa wa kipindupindu lakini kutokana na mwingiliano uliopo, hatua za kutosha zisipochukuliwa ugonjwa huu unaweza kuingia na kuenea ndani ya muda mfupi.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa ugonjwa huu unasababishwa na vimelea vya bakteria vinavyoitwa Vibrio Cholera na huambukisha kupitia kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya ugonjwa huo na dalili zake ni kuhara mfululizo, kutapika, ngozi kusinyaa na kuhema haraka haraka.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa