Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefunga mafunzo ya mfumo wa GoTHOMIS iliyoboreshwa kwa Maafisa Tehama na Watumishi wa Sekta ya Afya na kuwataka kuhakikisha kuwa Mkoa wa Mara unaongoza katika matumizi ya mfumo huo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Mtanda amewataka watumishi hao kuhakikisha mfumo wa GotHOMIS ulioboreshwa unafungwa na kutumika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara kabla ya Desemba, 2024.
“Mimi ninataka Mkoa wa Mara uonyeshe mfano wa kuigwa katika matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS ulioboreshwa ili mikoa mingine waje kujifunza Mkoa wa Mara, na hiyo inawezekana tukiamua” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vina vifaa vya Tehama vinavyohitajika kuwezesha mfumo huo kufanya kazi kwa ufanisi.
Amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanapanga ratiba za kufanya mafunzo na kufunga mfumo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma katika Halmashauri zao.
Mhe. Mtanda pia amewataka watumishi wa umma kujiwekea malengo na kufanyakazi kwa bidii ili kuyatimiza malengo ya kiutumishi na mtu binafsi.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Tehama kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bwana Mark Tanda ameeleza kuwa kwa sasa mfumo huu umeboreshwa na hauhitaji kufungwa mitambo ya Tehama katika kila kituo, badala yake vituo vitahitajika kuwa na vitendea kazi na mtandao tu kuweza kuutumia.
Bwana Tunda ambaye alikuwa ni mmoja kati ya wakufunzi wa mafunzo hayo ameeleza kuwa mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa taarifa za afya kutoa ngazi ya kutolea huduma za afya pamoja na ukusanyaji wa mapato katika vituo vya afya.
“Mfumo huu utaiwezesha Serikali kufuatilia dawa tangu zinavyotoka Bohari ya Madawa (MSD), Mikoa, Wilaya hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya” amesema Bwana Tanda.
Bwana Tanda ameeleza kuwa faida nyingine ya mfumo huu, utaviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya kufanya shughuli zake bila kutumia karatasi (paperless) na huduma zote kutolewa kupitia mfumo ikiwa ni pamoja na rufaa ya mgonjwa kwenda kituo kikubwa cha kutolea huduma.
Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya (GoTHOMIS) ni mfumo wa kukusanya mapato na taarifa katika vituo vya kutolea huduma za afya umeanza kutumika hapa nchini muda mrefu lakini kwa sasa umeboreshwa na kuhitaji mafunzo kwa watumiaji wake na hususan watumishi wa Sekta ya Afya na Maafisa Tehama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa