Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefanya ziara katika Wilaya ya Butiama na kuiagiza Mamlaka ya Maji Mgango- Kiabakari kuhakikisha maji katika mradi wa Maji wa Mgango-Kiabakari Butiama yanatwafikia wananchi kuanzia tarehe 10 Machi, 2024 kama walivyoahidi.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo wakati akiendelea na ziara yake kukagua ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Maji Mgango Kiabakari katika eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama na kuongeza wananchi wa Wilaya ya Butiama wamechoka taarifa nzuri, wanataka maji ya uhakika.
“Mimi na Wananchi wa Butiama tumechoka taarifa nzuri za maendeleo ya mradi, kwa sasa kinachohitajika ni maji safi na salama kutoka katika mradi huu uliotumia fedha nyingi kutekelezwa” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Bwana Mtanda ameahidi kuzungumza na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili waweze kuleta vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya mradi huo kuanza kufanyakazi mapema ili wananchi waweze kuepukana na adha ya kukosa maji safi na salama.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, ujenzi wa jengo la Uhamiaji Wilaya ya Butiama na ujenzi wa jengo la Polisi Wilaya ya Butiama na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama.
Akiwa katika miradi hiyo, Mhe. Mtanda amewataka wataalamu kutekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi kwa wakati na kuacha tabia ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila ya sababu za msingi.
Mhe. Mtanda amehitimisha ziara yake kwa kuzungumza na wakazi wa Kijiji cha Kiabakari, Kata ya Kukilango na kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuweka miundombinu ya dampo na vyoo katika eneo hilo.
Awali, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mgango Kiabakari Mhandisi Cosmas Sanda ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa shilingi bilioni 70.5 kwa sasa umefikia asilimia 97 ya utekelezaji wake.
Mhandisi Sanda ameeleza kuwa kwa sasa majaribio ya mitambo ya kusukuma maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matenki unasubiria TANESCO wakamilishe kufunga umeme na wameahidi kufunga na kuleta vifaa vilivyosalia ndani ya wiki moja kuanzia leo.
Bwana Sanda ameeleza kuwa kwa mpangokazi na mkakati uliopo, Mamlaka hiyoinategemea wananchi wa Wilaya za Musoma, Bunda na Butiama kuanza kupata maji mara baada ya TANESCO kukamilisha ufungaji wa umeme katika maeneo hayo.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa alipata fursa ya kusikiliza na kushughulikia kero na changamoto za wananchi wa eneo hilo na kuwapongeza wananchi kwa shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa