Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ameongoza kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Mara na kusistiza mahusiano na mawasiliano baina ya viongozi wa Serikali, Vyama, watendaji wa Serikali na wananchi katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi zikiwemo barabara.
“TANROADS, TARURA, SENAPA na Mamlaka za Serikali za Mitaa mfanyekazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha barabara zote zinapitika mwaka mzima ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao bila usumbufu” ameelekeza Mhe. Mtanda.
Aidha, amewahakikishia wajumbe wa kikao hicho kuwa Serikali yaw a Mkoa wa Mara itapeleka ombi maalum kwa Wizara ya Ujenzi ili bajeti ya barabara ya Mkoa iweze kuongezwa kama ilivyoamliwa katika kikao cha bodi hiyo.
Aidha, amewahakikishia wajumbe kuwa Serikali ya Mkoa inafuatilia kwa ukaribu ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ukarabati wa uwanja wa ndege wa Musoma, ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali zote za Halmashauri ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati.
Mhe. Mtanda ameziagiza Kamati za Usalama za Wilaya zote za Mkoa wa Mara kushughulikia changamoto ya wizi wa betri katika taa za sola zilizofungwa katika barabara zinazopita katika miji mbalimbali Mkoani Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya barabara hususan barabara zinazounganisha Wilaya za Mkoa wa Mara.
“Barabara ndio siasa yenyewe, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kuboresha barabara, wananchi hawatatuelewa bila barabara nzuri, tuhakikishe barabara zetu zinapitika muda wote ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao bila ya usumbufu” amesema Bwana Chandi.
Amezipongeza TARURA na TANROADS kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuziomba mamlaka hizo kuhakikisha barabara za Mkoa wa Mara zinapitika kwa wakati wote hasa zinazounganisha kati ya Wilaya na Wilaya.
Aidha, ameitaka Serikali ya Mkoa kufuatilia kwa ukaribu ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma na kuhakikisha Mkandarasi analipwa kwa wakati ili uwanja huo uweze kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe waliozungumza katika kikao hicho wameipongeza TARURA na TANROADS kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Mkoa wa Mara hata hivyo wameutaka Mkoa kupeleka maombi maalum ya kuongeza bajeti ya barabara za lami.
Akichangia katika kikao hicho, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo, Mbunge wa Jimbo Musoma Vijijini ameutaka Mkoa kuunda kamati ya Bodi ya Barabara ili kufanya tathmini ya barabara na mahitaji ya barabara za lami kwa Mkoa na kuziwasilisha Serikalini.
“Sisi wabunge tupewe taarifa za wasilisho hilo ili na sisi kwa nafasi zetu tukapambane kupata barabara zaidi za lami katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Muhongo
Taarifa ya Wakala wa Barabara (TANROADS) zimeonyesha kuwa wakala una barabara kuu kilomita 219.67 zenye lami na kilomita 190.06 za changarawe; barabara za mikoa kilimota 163.88 zenye lami na kilomita 789.93 za changarawe na barabara zilizokasimiwa kilomita 63.38 za changarawe wakati TARURA ina mtandao wa barabara kilomita 4559.08, madaraja 139, makalavati 2613.
Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini, Mwenyekiti na Katibu wa CCM Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wabunge, Meya wa Manispaa ya Musoma, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri, Mwenyekiti wa TCCIA, Mwenyekiti wa Wakandarasi.
Wengine waliohudhuria ni Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, watendaji wa TANROADS, TARURA, TEMESA, SENAPA, na wakuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Mara na Kanda Maalum ya Tarime/ Rorya na watendaji wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa